Azam FC yasajili washambuliaji wawili

Uongozi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC,imeingia mkataba na washambuliaji nyota kutoka Ghana, Samuel Afful na Yahaya Mohammed.

Azam Fc


Zoezi la kuingiana mikataba limehudhuriwa na baadhi ya viongozi wakuu wa timu wakiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Meneja Mkuu, Abdul Mohamed, Kocha Mkuu Zeben Hernandez pamoja na wakala anayewasimamia wachezaji hao, Kingsley Atakorah, ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Adom Wonders Academy ya nchini Ghana.

Wakati Afful, 20, akisaini mkataba wa miaka mitatu, Mohammed naye amesaini kandarasi ya miaka miwili tayari kabisa kuanza kuitumikia timu hiyo yenye maskani yake Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Afful ambaye mpaka sasa yumo katika vikosi vya timu za vijana za Ghana chini ya umri wa miaka 20 na 23, anajiunga Azam FC akitokea timu ya Sekondi Hasaacan ya Ghana, ambayo aliifungia mabao tisa msimu uliopita.

Moja ya rekodi yake ni kuifungia bao muhimu timu ya Taifa ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 (U-20) mwaka jana dhidi ya Zambia kwenye ushindi wa mabao 2-1, lililoipa nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini New Zealand, baada ya kutinga nusu fainali ya Mataifa ya Afrika kwa Vijana (U-20) zilizofanyika Senegal mwaka jana.

Mohammed, 28, ambaye ni mshambuliaji mzoefu anayetokea Aduana Stars, alikuwa ni mfungaji bora namba mbili wa Ligi Kuu ya Ghana msimu uliopita akifunga mabao 15, pungufu ya mabao mawili na kinara Latif Blessing (Liberty Proffessional) aliyetupia 17.

Chanzo: BBC