Profesa Joyce Ndalichako: Ukidanganya kuwa yatima kupata mkopo - Jela inakuita

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa baada ya uhakiki wa vyeti vya vifo vilivyowasilishwa na wanafunzi wanaoomba mikopo wakidai kwamba ni yatima, watakaobainika kupeleka vyeti vilivyoghushiwa watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.+



Hatua hiyo imekuja baada ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) hivi karibuni kubaini uwepo wa baadhi ya wanafunzi ambao wamewasilisha vyeti feki vya vifo vya wazazi wao ili waonekane kama ni watoto yatima, huku wakihitaji kupewa kipaumbele cha kupatiwa mkopo.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa elimu jana Dar es Salaam, Profesa Ndalichako alisema kwa wanafunzi ambao wanatambua kwamba walipeleka vyeti feki vya vifo na ripoti za daktari kuonesha kwamba wana magonjwa mbalimbali ambayo wanastahili kupewa mkopo, wajisalimishe kuepuka usumbufu watakaoupata. “Timu yetu inaendelea na uhakiki na ripoti itakapokamilika kwa wale wanafunzi watakaobainika wameghushi vyeti vya vifo hilo ni kosa la jinai hivyo watashitakiwa,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema wapo watu wanaosema hii ni serikali ya uhakiki, na kueleza kwamba Watanzania wamezoea kudanganya hivyo wanachokifanya ni kujiridhisha ili mtu apate haki inayostahili na si vinginevyo. Alisema kama mtu ni yatima basi awe yatima kweli kweli, lakini wameona dalili kwa watu wanaoghushi ripoti za daktari na vyeti vya vifo ili waombe mikopo.

Aidha, alisema timu ya kukagua vyuo vyote nchini ikikamilisha ripoti yake vyuo ambavyo havitastahili kutoa kozi fulani au kutoa mafunzo yote, vitafungiwa. Alisema baada ya vyuo hivyo kufungwa serikali itachukua jukumu la kuwapeleka wanafunzi katika vyuo vingine ili kuendelea na masomo yao. “Utaratibu wa sasa ni kwamba wanafunzi wanaomba kujiunga na masoko kupitia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) hivyo endapo kutakuwa na vyuo vimefungiwa kutoa elimu jukumu la wanafunzi waliopo litachukuliwa na serikali kuona watawapeleka wapi wanafunzi waliopo,” alifafanua Profesa Ndalichako. 

#HabariLeo