Wafanyakazi wizarani kuhamia Dodoma Januari

WIZARA ya Katiba na Sheria imeanza utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kuhamia mjini Dodoma kabla ya Februari mwakani.



Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome awamu ya kwanza ya watumishi wa wizara hiyo inategemea kuondoka jijini Dar es Salaam Januari kwenda Dodoma. “Kuhamia Dodoma haina mjadala, si sisi tu, ni wizara zote, awamu ya kwanza watawasili Dodoma kabla ya Februari. Watumishi wakaobaki watakwenda katika awamu zitakazofuata ambazo mtajulishwa baadaye," amesema Profesa Mchome.

Katibu huyo, aliwataka watumishi wote wa wizara hiyo kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma.

Awali, tangazo la wizara hiyo lilisambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu orodha ya watumishi wake wanaohamia Dodoma kuwa ipo tayari na wataondoka Januari.

Profesa Mchome alisema mambo mengine ni ya ndani na asingependa kuyazungumza wazi lakini alisisitiza kuwa, kikubwa kuhamia Dodoma ni lazima na itafanyika kwa awamu hadi kukamilika mwaka 2018.

#HabariLeo