Afya: Matunda na mboga za majani kumkinga mama mjamzito

Dk Hamis Shaabani daktari bingwa wa upasuaji wa mishipa ya fahamu kutoka Taasisi ya mifupa(MOI) ameyasema hayo leo wakati wa zoezi la ufungaji upasuaji wa vichwa vikubwa na migongo wazi katika hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma
Dk Hamis alisema kuwa utafiti uliofanywa na Taasisi ya MOI mwaka 2002 unaonyesha zaidi ya watoto 4800 huzaliwa kila mwaka wakiwa na maradhi ya vichwa vikubwa na migongo wazi na kati yao 500 pekee ndiyo wanaoweza kufika hospital na kupatiwa matibabu.
Akizungumzia chimbuko la maradhi hayo Dk Hamisi alisema kuwa watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi wanaweza kuzaliwa nacho au kupata siku chache baada ya kuzaliwa.
“Kwa wale wanaozaliwa na maradhi hayo ni kwasababu ya upungufu wa virutubisho ambavyo mama mjamzito anatakiwa avipate kabla ya kushika mimba virutubisho hivo vinapatikana kwenye matunda,mboga za majani, mayai na vyakula vyote vyenye protini, pia maradhi ya mgongo wazi husababisha watoto kupooza na kushindwa kutumia miguu yao,”alisema
Alisema mpaka sasa kwa Mkoa wa Kigoma jumla ya watoto 48 walihudhuria clinic na wameshawafanyia upasuaji jumla ya watoto nane wenye vichwa vikubwa sita na wawili wa mgongo wazi.
Ofisa habari wa GSM Foundation Khalfani Kiwamba alisema kuwa taasisi yao iliamua kudhamini matibabu ya maradhi ya vichwa vikubwa na migongo wazi baada ya kuelezwa changamoto mbalimbali za matibabu ya maradhi hayo na uongozi wa Taasisi ya MOI.

Anastazia Mtilili mkazi wa kijiji cha Minyinya Wilaya ya Kibondo akiongea kwa niaba ya wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa upasuaji wa maradhi ya vichwa vikubwa na mgongo wazi aliwashukuru timu nzima ya madaktari hao pamoja na Taasisi ya GSM kwa msaada huo wa matibabu waliowapatia wa watoto wao bure.
Aliiomba jamii kuacha kuhusisha maradhi hayo na mila potofu za imani za kishirikina au mikosi kwenye familia hali inayofanya akina mama au baba kutelekezewa watoto.
Aliwaomba pia wataalam hao wasogeze huduma hiyo karibu na jamii hasa maeneo ya vijijini ambapo wapo watoto wengi wenye maradhi hayo wanateseka na hawana msaada.
“Nawaomba wazazi wenzangu hasa akinamama sababu sisi ndiyo tunakaa na watoto kwa muda mrefu ndiyo tunaoweza kugundua mabadiliko ya mtoto pia tusisikilize maneno ya dhihaka ya watu wa pembeni maradha haya yanatibika kabisa”alisema mzazi huyo
Kaimu Katibu tawala wa Mkoa wa Kigoma Samwel Mtenga aliwashukuru madaktari pamoja na shirika la GSM Foundation kwa udhamini huo wa matibabu bure kwa watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi.
“Nawapongeza timu nzima ya GSM Foundation kwa uamuzi wenu huu wa kuja kuwapatia huduma hii ya upasuaji watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi,Mkoa wetu upo pembezoni wazazi wengi wanashindwa kupeleka watoto wao muhimbili au Bugando kwasababu ya umbali na gharama”alisema
Pia aliwataka wazazi wenye watoto wenye maradhi hayo wasione aibu kuwapeleka hospitali ili waweze kupatiwa matibabu bure.