MBUNGE wa Mtera mkoani Dodoma, Livingstone Lusinde (CCM) amehojiwa na Polisi kwa madai amekuwa na tabia ya kuwachochea wananchi wake, kujichukulia sheria mkononi katika mambo wasiyokubaliana nayo, jambo lililosababisha kuuawa kwa watafiti watatu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian Arusha (SARI) ndani ya jimbo lake.
Pia imebainika kuwa watafiti hao, ambao waliuawa na wananchi kwa kucharangwa kwa rangwa kwa mapanga na shoka katika Kijiji cha Iringa Mvumi, walikuwa na barua ya kuwatambulisha kutoka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kwenda kwa mtendaji wa kijiji hicho.
Habari za uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya Polisi Mkoa wa Dodoma, zilithibitisha kwamba mbunge huyo aliitwa jana kuhojiwa kutokana na kudaiwa huwa anashiriki kuwachochea wananchi wake, kuchukua sheria mkononi kwa mambo ambayo hawakubaliani nayo. “Ni kweli mbunge tumemwita asubuhi na kumhoji kuhusu taarifa hizo, tunashukuru ametupa ushirikiano, na kikubwa tulichokuwa tunahitaji kutoka kwake ni hizi taarifa za yeye kuhamasisha wananchi wake kujichukulia sheria mkoanoni,” kilisema chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Polisi Dodoma. Mbunge akanusha kuchochea Lusinde alipoulizwa kuhusu kuhojiwa na polisi jana alikataa. “Nihojiwe kwa jambo gani? alihoji mbunge huyo. “Ni kweli nilienda polisi asubuhi, lakini nilienda pale kuwaona viongozi wanaoshikiliwa na polisi, maana kuna diwani na mwenyekiti wa kijiji, hawa ni viongozi wenzangu lazima niwaone, lakini sikwenda kuhojiwa na polisi,” alisema Lusinde.
“Tangu uchaguzi uishe sijawahi kukanyaga kijijini hapo huo uchochezi nimeufanya saa ngapi? Aliongeza, “Kuna wataalamu wa maji na miradi mingine wanafika kijijini hapo hawajawahi kupigwa. Mimi ni mbunge nitaanzaje kuwachochea wananchi wangu? Kwa kweli huo ni uongo na uzushi dhidi yangu." #HabariLeo