“TUTACHUKUA HATUA ZA KISHERIA DHIDI YA WATU WANAOJIITA BODI YA WADHAMINI YA CHAMA”

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



“TUTACHUKUA HATUA ZA KISHERIA DHIDI YA WATU WANAOJIITA BODI YA WADHAMINI YA CHAMA”
Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi CUF inawajulisha wanachama na wananchi wote kwamba waipuuze taarifa ya watu waliokutana leo tarehe 04/10/2016 katika Ofisi Kuu ya chama Buguruni na kujitangaza kuwa wao ni Bodi ya Wadhamini ya CUF.

Bodi ya Wadhamini ya chama inapenda kuujulisha umma kuwa inaundwa kutokana na Kifungu cha 21 (1) na (2) cha Sura 258 ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Political Parties Act, Cap 258) na ibara ya 98 (1 – 6) ya Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014) na ina wajumbe tisa (9) ambao ni:
1. Abdallah Said Khatau – Mwenyekiti (Bara – Masasi),
2. Ali Mbarouk Suleiman – Makamu Mwenyekiti (Zanzibar),
3. Mohamed Nassor Mohammed – Mjumbe (Zanzibar),
4. Dr. Juma Ameir Muchi – Mjumbe (Zanzibar),
5. Zakaria Kwangu – (Bara – Magu) - kwa sasa Mgonjwa.
6. Yohana Mbelwa – (Bara – Kilindi) – ana dharura
7. Peter Malebo – (Bara – Geita),
8. Amin Salum Mrisha – (Bara - Moshi)
9. Joran Bashange  - (Katibu wa Bodi – Bara)

Bodi ya Wadhamini ya CUF ilifanya kikao chake Zanzibar tarehe 02 Oktoba 2016 na kuhudhuriwa na wajumbe 6 kati ya 9 na kwa mujibu wa Katiba ya CUF ilitimiza akidi na kufanya maamuzi mbalimbali. Mjumbe mmoja Ndugu. Yohana Mbelwa alitoa udhuru kwani ana matatizo. Hata hivyo Bodi ya Wadhamini ya CUF imeshangazwa kuona mitandaoni picha inayozunguka ikieleza kuwa “ kuna Bodi nyingine ya Wadhamini ya CUF” imekaa leo hii Buguruni.

Bodi ya Wadhamini ya CUF imeichunguza picha hiyo na kujiridhisha kuwa wapo watu wawili ambao ni wajumbe halisi wa Bodi ya Wadhamini ya Chama ambao ni  Peter Malebo  wa (Tanzania Bara – Geita) na Amin Salum Mrisha  wa (Tanzania Bara - Moshi).

Bodi ya Wadhamini ya CUF imegundua kuwa wajumbe hao wawili wamejiitishia “bodi feki” yao kwa kufuata mkumbo wa baadhi ya wanachama wanaojaribu kupingana na chama kwa kufuata maelekezo ya mtu aitwaye Ibrahim Lipumba ambaye ameshafukuzwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
Hata hivyo, Bodi ya Wadhamini inapenda watanzania wafahamu kuwa, wajumbe hao wawili ambao hawatimizi akidi ya watu watano na ambao wameitwa kwenye kikao feki hawawezi kubadilisha kitu chochote katika maamuzi ya Bodi halisi ya Wadhamini ya CUF iliyokwishakutana tarehe 02 Oktoba na maamuzi yake kutangazwa na Vyombo vya Habari tarehe 04 Oktoba 2016.

Kwa sababu Bodi ya Wadhamini ya The Civic United Front ipo kisheria, inatoa tahadhari kwa watu wote wanaotumiwa kwa namna moja ama nyingine, waache mara moja kulitumia jina la bodi hiyo kujiitishia vikao feki na kuita vyombo vya habari kujitangazia mambo ambayo hawakutumwa na Bodi.

Pia, bodi inazichunguza picha za wanachama wa CUF waliosimamishwa na ambao pia wamejitambulisha kama Wajumbe wa Bodi ya Chama na itachukua hatua za kisheria dhidi yao kwani wanatenda makosa ya jinai kwa kujiita wajumbe wa Bodi huku wakijua wanachofanya ni makosa. Bodi inaendelea na shughuli zake kama kawaida katika kusimamia maamuzi yaliyotangazwa na vyombo vya habari tarehe ya leo.

Abdallah Said Khatau (0787482388)
MWENYEKITI WA BODI.
Joran Lwehabura Bashange
KATIBU WA BODI.