Bodi ya wakurugenzi ya Shirika la ndege nchini (ATCL), limemtaka mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo kuwaondoa katika nafasi zao za kazi wakurugenzi wote katika menejimenti ya shirika hilo ili kuongeza ufanisi wa kazi.
Ndege ATCL |
Akizungumzia taarifa ya maazimio ya kikazi cha wakurugenzi wa bodi ya shirika hilo katika mkutano na waandishi wa habari Ijumaa hii jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa bodi hiyo Mhandisi Emmanuel Korosso amesema wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na wakurugenzi na menejimenti hiyo kuwa na utendaji usioridhisha.
“Imeamuliwa wakurugenzi wote katika menejiment ya ATCL na baadhi ya mameneja waondolewe kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utendaji dhaifu viwango vya elimu visivyokidhi matakwa ya nafasi zao ya uadilifu. Wakurugenzi wengi wamekuwa wakikaimu nafasi hizo. Tumeamua wakurugenzi wanaokaimu nafasi hizo warudishwe katika nafasi zao za chini ambazo sio za menejimenti au wahamishiwe katika vituo vingine vya mkoani,” alisema Koroso.
“Bodi pia imemuagiza Mtendaji Mkuu mara moja kutangaza nafasi za wakurugenzi na pia nafasi za mameneja zilizo wazi kwa kufuata muundo wa muda uliopitishwa na bodi. Mtendaji mkuu pia ameagizwa kutangaza nafasi zote ambazo anaona kuwa kuna umuhimu wa kutokana na utendaji usioridhisha kwa wafanyakazi wanaoshikilia nafasi hizo.”