DKT, KITILA MKUMBO: Kwa nini Watu/wanasiasa hujiunga na Vyama vya Upinzani Tanzania?

Sababu zinaweza kuwa nyingi lakini kwa maoni yangu tunaweza kuzigawa sababu hizi katika makundi makubwa matatu yafuatayo:

KITILA MKUMBO


a) Kujiunga na upinzani kwa nia ya kushiriki kujenga chama mbadala kiitikadi, kifalsafa, kisera, kimkakati na kiuongozi. Hii inamaanisha kuwa, kwa kuamini katika uwepo wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na faida zake kwa ustawi wa nchi, unaitikia wito uliopo ndani ya moyo wako wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taasisi mbadala za kisiasa ili kuleta ushindani wa kweli wa kisiasa na kuwapa wananchi/wapiga kura chaguo halisi wakati wa uchaguzi. Ukijiunga na chama cha upinzani kwa sababu hii ni vigumu, na pengine haiwezekani, kuhama na hasa kujiunga tena na chama tawala kwa sababu kiu hii huwa haishi.

b) Kukerwa na matendo ya viongozi wa chama tawala (reactionary factors): Hapa mtu hujiunga na chama cha upinzani kama njia ya kuonyesha hasira ya kukerwa na baadhi ya viongozi katika chama tawala kutokana na matendo yasiyoridhisa. Watu wa kundi hili hujuta muda mfupi baada ya kujiunga na upinzani na mara baada ya hasira kwisha. Mambo mawili yanaweza kutokea kwa watu waliopo katika kundi hili. Mosi, inawezekana watu katika kundi hili wakakua kiimani na hatimaye kuingia katika kundi la kwanza. Pili, ama hasira zitaisha au wabaya waliowafanya wahama chama tawala watakuwa wameshaondoka katika chama chao cha awali. Kimsingi watu waliopo katika kundi hili la pili hawajawahi kuhama chama chao cha zamani kiroho. Walihama kimwili tu. Katika hatua hii, ni suala la muda tu kabla watu wa aina hii hawajaresha miili yao ili kuungana na roho zao katika chama chao cha zamani.

c) Fursa za kisiasa na maisha: Hii hutokea pale ambapo mwanasiasa huona kwamba hana fursa ya kushinda katika chama tawala kwa kuwa uwezo wake ni mdogo wa kuweza kukabiliana na ushindani huko. Hivyo hujiunga na upinzani kwa ajili ya kusaka fursa na uwezekano wa wao kushinda katika nafasi za kugombea au kuteuliwa. Wengi wa waliojiunga na upinzani kwa sababu hii huishia kurudi tena katika chama tawala pale wanapokosa fursa walizozifuata katika upinzani. Hata hivyo, katika kipindi walichokuwa upinzani watu hawa huwa wametengeneza mtaji fulani wa kisiasa unaowawezesha kuvuma aghalabu kwa muda mara wanapoamua kurejea chama tawala.  Aidha, watu hawa huhisi kwamba kuna fursa za maisha kupitia uteuzi na/au makandokando yanayoambatana na harufu njema ya chama tawala. Hivyo, ili kujijengea uhalali huko waendako, watu katika kundi hili huandaa mazingira ya mbwembwe na kuonyesha kwamba kuna tetemeko kubwa huko walikotoka kwa sababu ya kuondoka kwao. Huko zamani watu wa namna hii walipokelewa kwa mbwembwe na wakubwa wa chama tawala.

Kwa ujumla, uzoefu Tanzania unaonyesha kuwa ni vigumu kuendelea kuwa mwanasiasa kwa mpinzani kurudi CCM. Mtu pekee aliyeendelea kuwa mwanasiasa hata baada ya kurudi CCM ni Steven Wassira. Ndiyo maana huyu kuna wakati aliitwa ‘Mr Tyson’!

Ukishaelewa hivi, huna sababu ya kugombana na au kumnunia mtu anayehama chama cha siasa zaidi ya kumtakia kila la heri huko aendako!