Siku moja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuagiza Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akamatwe kwa kushindwa kuhudhuria kortini, mbunge huyo amedai hana taarifa hizo hivyo hawezi kujisalimisha popote.
Lissu ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, alidai atajisalimisha tu kwenye vyombo vya dola au kwenda mahakamni ikiwa atapelekewa barua aliyoandikiwa na mahakama na kutiwa saini na kugongwa muhuri na hakimu.
“Kaka, mimi siwezi kufanyia kazi za magazeti katika masuala ya kisheria, nipo hapa ninaendelea na shughuli zangu kama kawaida na kama mnavyoniona niko katika kuwawakilisha wananchi wa jimbo langu,” alieleza Lissu.
Mwanasheria huyo mkuu wa Chadema alitoa maelezo hayo jana alipohojiwa kuhusiana na habari zilizoandikwa na vyombo vya habari, kwamba Mahakama ya Kisutu juzi iliagiza mbunge huyo akamatwe baada ya kushindwa kuhudhuria katika kesi inayomkabili.