Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia anefanyiwa operesheni ambayo imechukua saa nne hadi kukamilika kwake katika Hospitali ya Zydus Ahmedabad Gujarat nchini India. Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, Mkoa wa Kilimanjaro alipelekwa India Novemba 10 kwa matibabu ya mguu huo ambao umekuwa ukimsumbua muda mrefu na alifanyiwa operesheni Novemba 14.
Akizungumza kwa simu kutoka India, Dk Baltazar Mbatia ambaye ni mdogo wa mbunge huyo amesema kaka yake alifanyiwa upasuaji kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana.
“Wakati tunakuja hapa India, kaka (Mbatia) alikuwa akilalamika sana juu ya maumivu aliyokuwa akiyapata katika mguu wake. Hata hivyo tunamshukuru Mungu sasa anaendelea vyema baada ya upasuaji wa mafanikio kukamilika,” amesema huku akisisitiza kuwa maadili ya udaktari hayaruhusu kusema kwa undani mgonjwa anaumwa nini isipokuwa mhusika mwenyewe au mamlaka husika atakazoziagiza.
“Kabla ya kuzungumza na wewe, niliongea na Mheshimiwa (Mbatia) kaniambia anaendelea vizuri na amewataka Watanzania kuendelea kumwombea,” amesema Dk Mbatia.
Mkuu wa Kitengo cha Habari Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya amesema Mbatia anatarajiwa kurudi Tanzania katikati ya wiki ijayo baada ya matibabu yake kukamilika.