Mbunge Halima Mdee ataka Kamati Teule sakata la Uda

SUALA la uuzwaji wa hisa za Shirika la Usafiri la Jiji la Dar es Salaam (UDA), limeibuka tena bungeni baada ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) kutaka suala hilo liundiwe Kamati Teule ya Bunge.

UDA


Pamoja na suala hilo la UDA kuibuliwa na Mdee, pia wabunge wengi wameitaka serikali kuongeza fedha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili itekeleze majukumu yake vizuri zaidi.

Mdee aliyeeleza historia ya UDA na namna linavyozingirwa na ukakasi, alisema atawasilisha hoja binafsi bungeni kuomba kuundwe kamati hiyo Teule ya Bunge kuchunguza suala hilo.

Wakati Mdee akieleza hayo, Waziri wa Nchi, Ofis ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene, alisema bungeni kuwa serikali imekwenda hatua kwa hatua kuhusu UDA kwa kushirikiana na Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC) na tayari kamati hiyo imeagiza taarifa fulani ili kukamilisha suala hilo na kamati italeta taarifa bungeni.

Mdee alikuwa akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ya kuanzia Juni 30, 2014 hadi Juni 30, 2015 pamoja na ile ya Serikali za Mitaa (LAAC), ya mwaka 2013/14 na 14/15, jana bungeni mjini hapa.

Alisema yeye ni mjumbe wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam na baada ya kuona suala la UDA limeingizwa bungeni na mambo yanayohusiana na jiji yakitajwa na baadhi ya hoja kutaka Jiji livunjwe kutokana na kashfa ya kiwanda cha nyama, baadhi wanasahau kwamba yanayotokea sasa katika shirika hilo yalianza wakati wa CCM ikiliongoza Jiji hilo.

Alisema sasa wakati Ukawa wapo kwa wingi katika Jiji, wanataka kusafisha masuala yote ya ufisadi katika Jiji. “Nimesikia zile bilioni tano alizolipa Simon Group zinataka zipangiwe matumizi, naomba niwaambie sisi kama Jiji tunatambua mamlaka yetu, sasa kama hatujitambui na serikali inataka kuingilia sisi tunatambua mamlaka yetu,” alisema Mdee.

#HabariLeo