Prof Ndalichako atoa siku moja kwa bodi ya mikopo kufikisha fedha za mikopo vyuoni, ataka vyuo vianze kugawa fedha hizo mara moja Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema uchelewaji wa mikopo ya elimu ya juu umetokana na ucheleweshaji na ukamilishaji wa taarifa za matokeo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo umeathiri kasi ya kutuma fedha kwenye vyuo mbalimbali.
Prof. Ndalichako amelazimika kutoa ufafanuzi huo bungeni mjini Dodoma baada ya baadhi ya wabunge akiwemo mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete kuomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge akimtaka Waziri wa Elimu kutoa msimamo wa serikali juu ya hatma ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Aidha Prof. Ndalichako amesema serikali imeshapeleka zaidi ya shilingi Bilioni 71 kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo na watakaobainika kupata mikopo kwa njia ambazo siyo sahihi wataondolewa na fedha hizo zitaenda kwa wanaostahili.
Katika mwaka wa fedha 2015/16 Serikali ilitenga zaidi ya shilingi Bilioni 473 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ambapo hadi sasa wanafunzi wa mwaka wa kwanza 58,010 waliodahiliwa kati yao 21,190 tayari wameshapatiwa mikopo na kwamba serikali haijafuta mkopo kwa mwanafunzi yeyote.
Chanzo: ITV