Aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametunukiwa tuzo baada ya kutangazwa mshindi wa mwaka 2016 wa Taasisi ya Mafanikio ya Govan Mbeki (Govan Mbeki Lifetime Achievement Award), katika sherehe iliyofanyika usiku wa kuakia jana, kwenye Ukumbi wa International Convention Center (ICC) mjini Durban, nchini Afrika Kusini.
Profesa Tibaijuka, ambaye pia alipata kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN- Habitat), ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na ufanisi aliouonyesha, ikiwa ni pamoja na kuendesha mikakati na kampeni kubwa bila kuchoka ya kupambana na makazi duni na mazingira barani Afrika na duniani, wakati akiliongoza shirika hilo.
Waziri wa Maendeleo ya Makazi wa Afrika Kusini, Lindiwe Sisulu, ndiye aliyemkabidhi tuzo hiyo na cheti Profesa Tibaijuka, baada ya kutangazwa mshindi.
Profesa Tibaijuka, ambaye ni Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), ametunukiwa tuzo hiyo baada ya kuonyesha kuthamini mchango wake wakati akiwa UN Habitat, kati ya mwaka 2000-2010.
Kiongozi huyo, licha ya kujipatia sifa lukuki wakati akiliongoza shirika hilo la Umoja wa Mataifa na hivyo kumuandalia njia nyepesi ya kushinda ubunge Jimbo la Muleba mwaka 2010 na hata kuteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, hata hivyo, sifa hizo zilitiwa doa baada ya kuhusishwa kwenye mgawo wa fedha tata zilizochotwa kutoka katika akaunti ya Escrow.