HUKU kukiwepo na dhana ya kuwa kuna Watanzania wanaotorosha fedha na kuzificha katika mataifa mbalimbali ikiwemo Uswisi, hatua moja muhimu imefanyika katika kukabili suala hilo, baada ya serikali ya nchi hizo mbili, kusaini mkataba muhimu.
kufikiwa kwa makubaliano ya ushirikiano muhimu wa kisheria kwenye masuala ya jinai, unalenga kuwajengea uwezo makachero wa Tanzania, kuchunguza masuala mbalimbali ya kiuhalifu nchini Uswisi.
Mkataba huo umeenda mbali zaidi, kwa kuweka wazi kuwa kuanzia sasa makachero hao, wanaweza kuchunguza fedha za Watanzania zilizohifadhiwa nchini Uswisi, tofauti na awali ambapo sheria za nchi hiyo zilikuwa zinazuia.
Mkataba huo umesainiwa hivi karibuni wakati wa Maadhimisho ya miaka 50 ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uswisi. Uswisi ni nchi inayosifiwa kuwa na huduma bora za kibenki huku ikiwa na sheria kali zinazowalinda wateja wake.
Mkataba wa makubaliano hayo, ambao umeleta mwanga katika kukabiliana na usiri wa fedha hizo, ulisainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga na Balozi wa Uswisi nchini, Florence Mattli