Dar es Salaam. Mtandao wa Asasi za kiraia unajipanga kuanzisha upya majadiliano ili kusukuma kuanza kwa mchakato wa kutafuta katiba mpya ambayo watanzania wamekuwa wakiisubiri kwa muda mrefu.
Lengo la mtandao huo kabla ya kufikia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 Tanzania iwe imepata katiba mpya.
Akizungumza wakati mkutano uliozikutanisha asasi mbalimbali za kiraia Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olenguruma amesema wakati umefika sasa kwa watanzania kuanza kudai katiba.
Amesema katiba inayohitajika siyo itakayoegemea upande wa CCM wala ukawa bali ni ile itakayoainisha vitu wanavyotaka watanzania. “Katiba tunayotaka ni ya watanzania hatutaki wanasiasa waingilie kati kutuharibia mchakato wananchi wenyewe ndiyo wahusike katika hili:
Hii haimaanishi tunaikataa rasimu ya Warioba au katiba inayopendekezwa tunachotoka zote kwa pamoja ziunganishwe na katiba iliyopo na mawazo ya watanzania ili tutengeneze katiba itakayokubaliwa na wote, ”amesema
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi (Tucta) Gratian Mkoba amesema asasi za kiraia zina uwezo mkubwa wa kubeba ajenda mpya zitakazochangia kupatikana kwa katiba mpya. #mwananchi