'Boom' la wanafunzi wa vyuo limetoka rasmi

Tanzania shilingi


AKAUNTI za wanafunzi wa vyuo vikuu nchini zitakuwa zimeanza kunona baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kusema kuanzia jana imeanza kuingiza fedha za wanafunzi wote wa elimu ya juu ambao wamekidhi vigezo vya kupatiwa mikopo.

Wanafunzi 20,183 kati ya wanafunzi 58,010 ambao wamedahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ndio ambao wamepangiwa kupata mikopo na bodi hiyo baada ya kutimiza vigezo vyote vilivyowekwa. “Napenda kuwahakikishia waombaji kuwa boom limeanza kuingia leo, kwa kuwa fedha hizo zinapitia benki baadhi wanapata kesho na wengine siku zinazofuata, ila sisi tumeshatimiza wajibu wetu,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul Razaq Badru wakati akizungumza na gazeti hili jana.

Kwa idadi hiyo ya wanufaika wa mikopo iliyotangazwa na bodi, ni wazi kuwa wanafunzi wengine 37,827 hawatapatiwa mkopo kutokana na kukosa sifa ambao zimeainishwa na bodi hiyo.
Jumla ya wanafunzi 88,163 waliomba mikopo ya HESLB.