MACHIMBO YALIYOFUKIA WANNE PUGU FRESH YAGEUZWA KABURI


Shughuli ya uokoaji watu wawili waliobaki baada ya watu wanne kufukiwa katika kifusi katika machimbo ya kokoto yaliyopo eneo la Golani, Pugu Kigogo Fresh jijini Dar es Salaam umesitishwa baada ya kuonekana inaweza kugharimu maisha ya watu wengine.

Aidha eneo hilo limegeuzwa kuwa kaburi baada ya jitihada za kumuokoa kijana wa nne Boniface Pius (27) kushindikana kutokana na utete wa eneo lenyewe. Shughuli hiyo ya uokoaji imesitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema ambaye alikuwa eneo hilo kwa siku tatu na kufanikiwa kuwapata vijana watatu mmoja kati ya wanne akitoka akiwa hai.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la tukio, Mjema alisema, wametumia siku tatu na kiutaratibu kama muda wa saa 72 utapita na shughuli kushindikana ni lazima wasitishe shughuli hiyo.

“Tulianza shughuli hii kwa siku tatu zilizopita majira ya saa tatu na nusu asubuhi tuliweza kumtoa Rashid Fadhili (28) akiwa ameshakufa wakati tukiendelea na jitihada za kumpata Boniface tumeona hali ni mbaya kama serikali hatuwezi kuruhusu mtu, au kikosi kuendelea na shughuli hii kwa kuwa kuna hatari ya kuangukiwa na udongo hivyo zoezi limesitishwa na tumekubaliana na wazazi waite mchungaji kwa ajili ya kuendesha ibada katika eneo hilo, ”alisema Mjema.

Aidha Mjema alitangaza kufungwa kwa machimbo hayo na kutoa siku mbili kwa wachimbaji hao kuondoa vifaa vyao na baada ya hapo watalifunga na hakuna atakayeruhusiwa kuingia katika eneo hilo tena.
#haabarileo