GDP ya Manispaa Kigoma Ujiji kufikia tshs 1.5 trilioni

HALMASHAURI ya Kigoma Ujiji, inajipanga kufikia mwaka 2020, iwe na uchumi wa Sh trilioni 1.5 kutokana na miradi mbalimbali ya kilimo cha michikichi, soko kubwa la kimataifa la Ujiji na uvuvi.


Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam na Mshauri wa Masuala ya Uchumi, Paulsen Mrina katika mkutano kati ya viongozi wa Halmashauri ya Kigoma Ujiji akiwamo Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Kabwe Zitto na wananchi wa mkoa huo wanaoishi jijini humo wakati wakijadili rasimu ya mkakati wa uendelezaji mji huo.
“Tatizo la Mkoa wa Kigoma mzunguko wa fedha haupo, tukifanikiwa kuongeza mzunguko katika manispaa hiyo na mkoa kwa ujumla, maendeleo yatapatikana. Kigoma ni sehemu nzuri, wachapakazi, ardhi nzuri na masoko makubwa,” alisema Mrina.

“Hii itakuwa ni pamoja na kutengeneza ajira 100,000, kutengeneza miundombinu ya kuvutia wawekezaji na wananchi kuwa na pensheni,” alisema mchumi huyo.

Aidha, aliainisha sekta zilizopewa kipaumbele kuwa ni uchumi wa mawese, kilimo cha mpunga, uvuvi wa kisasa, usafirishaji na masoko, utalii, uchumi wa gesi na mafuta katika Ziwa Tanganyika, ingawa unachukua muda mrefu kuanza kuzalishwa.

Katika kilimo cha michikichi alisema, inatarajiwa kufikia mwaka huo zitakuwa zikizalishwa tani 80,000 ambazo ni sawa na Sh bilioni 50, lengo ikiwa ni kupanda miche 3,000, tofauti na sasa ambapo zinazalishwa tani 8,000 pekee.
Kuhusu uvuvi alisema, mabwawa ya manispaa hiyo ambayo yalikuwa hayafanyi kazi, yataanza kugawiwa kwa wananchi kwa lengo la kufugia samaki, na pia kufanya mazungumzo na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuruhusu boti za kisasa kuruhusiwa kufanya uvuvi.

Zitto alisema, utaratibu huo wa kuwashirikisha wananchi wa Kigoma waishio Dar es Salaam, umeanza sasa lakini utakuwa endelevu angalau mara moja kwa mwaka.
“Nikaona tukutane na kujadiliana maendeleo ya mji wetu, tunatarajia baada ya kukusanya mawazo leo, tutamuomba mshauri wetu aweke mawazo yetu kwa namna ambayo yanauzika kwa wawekezaji,” alisema Zitto.
Alisema baada ya hapo Oktoba 29, mwaka huu, watakutana na wawekezaji ambao ni wafanyabiashara wakubwa nchini pamoja na mabalozi wa nchi mbalimbali.

Katika mradi huo wa mji wa Ujiji, utawezesha wafanyabiashara kutoka nchi za jirani na Kigoma badala ya kufuata vitu China au Dar es Salaam, wapate bidhaa zote hapo baada ya wawekezaji kuleta bidhaa zao.
Alisema mradi wa pili ambao unatarajia kuingizia fedha manispaa hiyo ni kilimo cha michikichi, kutokana na mahitaji ya zao hilo duniani kuongezeka. Tanzania kwa sasa, inaagiza tani 50,000 za mawese kila mwezi ambazo ni sawa na tani 600,000 kwa mwaka.