Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imemuachia huru Kijana aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya uchochezi



Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imemuachia huru Kijana Allan Harold Mbando, mwenye miaka 23 mwanafunzi wa chuo cha maendeleo ya jamii Arusha (CDTI) baada ya kumuona hana hatia katika kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili.

Awali ilidaiwa katika mahakama hiyo kuwa mnamo tar.07 May mwaka huu, kupitia simu yake aina ya Tecno Y4 kijana huyo aliandika maneno ya uchochezi katika ukurasa wake wa Facebook akisema "Mwamunyange pindua nchi, haiwezekani wote wawe nje halafu hakuna aliyepewa mamlaka ya kukalia kile kiti"

Jeshi la Polisi na ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali walidai maneno haya ni uchochezi uliolenga kushawishi Jeshi kufanya mapinduzi wakati viongozi wakuu wa serikali walipokua nje ya nchi, kinyume na sheria ya mitandao no.14 ya mwaka 2015 kipengele cha 16.

Katika hukumu hiyo Mahakama imesema hakuna ushahidi wowote uliotolewa na Jamhuri na kuweza kudhibitisha kuwa maneno hayo yalilenga uchochezi.

Hata hivyo Jamhuri imeshindwa kuieleza Mahakama hiyo mtu aliyetajwa katika andiko hilo kwa jina la "Mwamunyange" ni nani, ana wadhifa gani na yupo nchi gani. Upande wa mashtaka pia ulishindwa kutaja nchi ambayo "Mwamunyange" aliambiwa apindue.!