Maoni ya Dr Slaa, Zitto na Josh Nassari baada ya malumbano kati ya Mkuu wa mkoa Arusha na Mbunge wa Arusha mjini

Siku ya jana katika sherehe ya kuweka Jiwe la msingi kwa ajili ya Ujenzi wa Hospitali ya Akina Mama na Mtoto kulitokea mvutano kati ya Mkuu wa Mkoa na Mbunge wa Arusha mjini na kuzua Taharuki kwa wageni na wafadhili wa mradi huo. Huku Mbunge akilalamika kuwa Mkuu wa mkoa wa Arusha kavuruga ratiba ya Hiyo ya Kuweka jiwe la msingi.



Maneno ya Zitto Kabwe baada ya tukio

Nakasirishwa sana kuona viongozi vijana wanafanya mambo ya hovyo. Mkuu wa mkoa wa Arusha mdogo wangu  Mrisho Gambo una dhamana zaidi Kwa vijana. Mnapofanya mambo ya kijinga mnaharibu nafasi ya vijana kuaminiwa zaidi. Kaa Na Mbunge Godbless Lema mnywe kahawa pale New Arusha Na muanze upya. Ndugu yangu Lema nashauri punguza munkari. Juhudi zako Arusha haziwezi kufutika kirahisi. Nakushauri kaa chini Na Mkuu wa Mkoa wako mpige mstari muanze Kazi upya Kwa pamoja.

Viongozi jiepusheni kuonyesha hasira zenu hadharani. Sio hekima.

Anaandika Mhe.Josh Nassari

Sina tatizo binafsi na Mhe. RC Gambo. Ila katika hili amepotoshwa naye akapotoka. Mimi ni mmoja wa waanzilishi wa ArDF tangu mwezi December 2010 nikialikwa na Mhe Lema. Ikumbukwe sikuwa Mbunge wakati huo. Si dhamira yangu kuandika mengi kwa sasa kwa kuwa nipo darasani. Lakini nimekumbuka namna tulivyokuwa tukihangaika na kufanya vikao usiku na mchana kutafuta Ardhi kwa ajili ya hospitali hii. Niliendelea kushiriki hata baada ya Kuwa Mbunge wa jimbo jingine kwa sababu nilijua huduma zingetumiwa na wana Meru pia na ukizingatia Kuwa Ardhi ilikuja kupatikana ndani ya Wilaya yangu ya Arumeru. Hizi ni baadhi ya picha za miaka 6 iliyopita. Wakati huo Gambo alikuwa mtumishi wa halmashauri. Na picha nyingine ya mwezi Mei 2015 wakati MOU ikisainiwa. 

Tumpe Kaisari iliyo ya Kaisari. ArDF, Lema, Mawala, Maternity Africa and Dada Happy Mwamasika deserved an acknowledgement. It doesn't hurt a thing. Naomba radhi kwa waliokwazika na tukio la jana. Lakini hii inaonyesha namna gani tulivyo na safari ndefu katika democracy and resilience!

Joshua Nassari (MB)

Anaandika Dr.Wilbroad Slaa (Katibu Mkuu wa zamani wa CHADEMA).


Mrisho Gambo,
Naamini hii ID ni ya kwako na hasa kwakuwa kwenye post unaonekana ukizungumza, napata uhakika kuwa ni wewe.

1) Mkuu wa Mkoa, nakuheshimu kwa kuwa cheo chako ni kikubwa sana. Hata hivyo, ulichokifanya leo na " propaganda unazopiga zimenifanya nikudharau na kukupuuza. Ningeliweza kuishia katika kukudharau na kukupuuza, lakini
2) Aibu uliyoiletea Taifa letu leo, inanifanya " nipige kelele" kuwa " siasa za maji taka siyo wakati wake huu.
a). Mhe.Mrisho Gambo, wewe kama Mkuu wa Mkoa unayo au mamlaka au vyombo vya dola kukusaidia kufanya utafiti wa maana kuliko aibu kubwa uliyoiletea Taifa letu mbele ya Wahisani/ Wafadhili wetu kupitia Maternity Africa. Hukufanya hivyo, umeamini propaganda kuliko busara na hekima. Kwa hilo siwezi kukusamehe wala kukuheshimu pamoja na cheo au vyeo vyote ulivyonavyo.

b). Mrisho Gambo, ungelikuwa wa busara iwapo ungelimwomba kiongozi au mwakilishi wa ADF (ulikuwa na uwezo wa kujua ADF ni nani na historiaya yake ni ipi- kwa kupenda propaganda hukufanya hivyo) au Mwakilishi wa Maternity Africa hasa Happy (ambaye alisaini pia barua ya kukualika kuwa mgeni rasmi, au hata Mhe.Mbunge Lema ambaye kimsingi ndiye chimbuko la upatikanaji wa Ardhi hiyo kutoka kwa Marehemu Advocate Mawala (Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi), na pia chimbuko la Upatikanaji mradi kutoka kwa wafadhili wetu.
Kutokupenda kushauriwa na hao wenye kujua mradi imekufanya "kuonekana juha" na " mwongo" kwa kuwa historia haifutwi kwa " propaganda za jukwaani". Lakini kwa bahati mbaya athari ya propaganda imeenda mpaka kuichafua Taifa letu kwa wahisani. Ujenzi ndiyo kwanza unaanza. Umeombwa kufanya "Ground Breaking ceremony", unadhani wawakilishi wa wahisani na hasa kule kwenye chimbuko la fedha wanapata picha gani ya Taifa letu.

c). Mrisho Gambo, busara na hekima ya kawaida ingelikuwezesha kuelewa barua ya mwaliko ambayo imesisitiza mara mbili hivi, kuwa wahusika ni taasisi isiyojihusisha na siasa. Wakasema mradi kwa muda sasa umekumbwa na matatizo yenye sura ya kisiasa. Ulipaswa kutafakari, kutafiti na kutafiti njia makini zaidi ya kuona wakina mama wajawazito, wenye fistula na watoto wachanga hawakosei au hata hawacheleweshewi kupata huduma hiyo kwa sababu za kipuuzi tu. Eti unasoma historia! Unaijua historia au unaota ndoto! 
Nimepiga kelele kwa kuwa ninaijua vizuri hiyo historia A to Z. Sikuambii ungeliniuliza, lakini wapo kwenye kikao hicho ambao wasingelihitaji kuisoma bali kuitoa kichwani historia hiyo, tangu kupatikana kwa Ardhi, mchakato wa kuchora ramani, kuisajili na kupata vibali vyote vya Kituo hicho cha Afya (japo kwa kweli ni hospitali, inaitwa kituo cha Afya tu kwa. Sababu za kisheria).

3) Mrisho Gambo, kwa hili Watanzania wa Arusha na wote wenye kujua ukweli hatutakusamehe kwa aibu uliyotupatia, na kujenga misingi ya kutufungia miradi mingine kwa wahisani wetu.
Kama una chembe dogo la busara:
a). Utakaa chini na kutafakari umekosea wapi.
b). Uwe na unyenyekevu uwaite wahusika wote ofisini kwako waombe wakupe " historia kamili" na wakupe mchakato mzima mpaka kufikia siku hii muhimu ya "Ground Breaking ceremony (uzinduzi wa Kazi ya ujenzi).
c). Ukipata Taarifa kamili, uwe na unyenyekevu, acha kiburi. Kiburi hakikusaidii wala haitasaidia jamii unayopaswa kuwatumikia (unless una malengo tofauti). Kwa unyenyekevu mkubwa Waombe msamaha Wahisani wetu kwa kuwaingiza katika " siasa ya Arusha" ambayo hawahusiki nayo; awaombe msamaha wakina mama, watoto na jamii ya Wananchi wa Arusha wapenda maendeleo kwa kuwachafua na kuwaletea vurugu kiasi cha kuifanya Arusha ionekane kila leo ni mahali pa vurugu, kumbuka vurugu husababishwa na viongozi wasiotumia busara na hekima. Uongozi ni busara na hekima siyo mabavu wala nguvu ya mamlaka.

Nimeyasema haya kwa uchungu mkubwa. Mimi siko kwenye siasa, na wala sina interest na siasa. Siangalii uso wa mtu. Kama ambavyo niliaga kuwa " Nastaafu Party Politics, lakini nitapiga kelele pale maslahi ya Taifa langu yanavyokanyagwa" nitakuwa mwendawazimu kunyamaza wakati mradi wa Tshs Takriban 9 Billioni unahatarishwa na upuuzi na uzembe wa kiongozi mmoja mwenye kuendekeza propaganda zisizo na msingi.
Nawaomba sana Radhi wahisani wetu. Mtuvumilie siyo kwa ajili yetu bali kwa ajili ya kina mama na watoto walengwa wa huduma itakayotolewa na " Kituo cha Mama na Mtoto" (propaganda kwamba Hospitali ni ya mke wa Lema zipuuzeni).

Happy, umevumilia mengi katika miradi mingi uliyofadhili na kuisimamia. Usirudi nyuma. Timiza ndoto yako iliyoanza katika umri mdogo sana. Matunda yanaonekana pamoja na vikwazo vya mara kwa mara vya wapinga maendeleo. Viongozi, " Tenganisheni siasa na Maendeleo" Watumikieni Watanzania bila kuangalia nyuso zao, mrengo wao. Siasa ni sayansi na siasa ni utumishi.

Dr.Wilbroad Peter Slaa via #Jamiiforums.!