BIASHARA YA MENO YA TEMBO YAMTUPA JELA MIAKA 25, FAINI SH 3.7 BILIONI

Tanga. Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga imemuhukumu kifungo cha miaka 25 ama kulipa faini ya Sh 3.7 bilioni mfanyabiashara, Charles Kijangwa baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo.



Hakimu Mkazi, Cresian Kisongo ametoa hukumu hiyo leo kwa Kijangwa ambaye aliruka dhamana tangu mwaka 2010, takribani miaka sita sasa.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kikosi cha kuzuia ujangili Kanda ya Mashariki na Pwani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Wilaya ya Lushoto kufanikisha jitihada za kumtafuta kwa kumkamata na kumkabidhi mahakamani hapo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Saraji Iboru alidai mahakamani kuwa mshtakiwa Kijangwa alikuwa akitafutwa na Serikali kwa muda mrefu tangu mwaka 2010 ambapo aliruka dhamana katika kesi ya uhujumu uchumi namba 6 ya mwaka 2007 iliyokuwa ikimkabili yeye pamoja na wenzake Michael Msuya na Nyaisa Makori.

#Mwananchi