Walimu 4 watumbuliwa kujihusisha na mapenzi na wanafunzi

WALIMU wanne wa Shule ya Sekondari Kitumbeine wilayani Longido Mkoa wa Arusha, wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi baada ya kutuhumiwa kujihusisha na mapenzi na wanafunzi wao.



Akisoma risala kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambaye yupo wilayani humo kwa ziara ya siku tano ya kukagua maendeleo na changamoto, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo alisema hivi sasa uchunguzi unafanyika, kubaini jinsi walimu hao walivyojihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao.

Chongolo alisema uchunguzi utakapokamilika na ikithibitika, watachukuliwa hatua za kinidhamu. Alisema pia kuwa kuna changamoto ya mimba ya utotoni, ambazo baadhi ya wazazi na walezi wao wamekuwa wakiwaozesha kutokana na mila.

Alisema serikali inafuatilia wazazi wenye tabia hiyo ya kuwaozesha watoto kwenye umri mdogo kwani tatizo hilo lipo kwa asilimia 13 katika jamii ya wafugaji.