Ujumbe wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa Chuo Kikuu UDSM




MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais mstaafu Jakaya Kikwete amekitaka chuo kikuu hicho (UDSM) kilinde hadhi yake ya kuendelea kuwa kiongozi katika utoaji wa elimu bora, ambayo itasaidia taifa kuwa na wataalamu wenye kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili kijamii.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana, Kikwete alisema hatua ya chuo hicho kufikisha umri huo ni wazi kuwa kimekomaa na kimetoka katika hatua mojawapo ya makuzi na kwenda nyingine, hivyo kinastahili kuwa chachu ya maendeleo kwa kutoa wahitimu wenye kuleta mabadiliko katika nchi.

Kikwete ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa mkuu wa chuo hicho, alisema licha ya chuo hicho kutoa mchango mkubwa kwa nchi ikiwa ni pamoja na kutoa viongozi wa nchi na wataalamu ambao wamekuwa msaada mkubwa katika kutunga sera za nchi, kinatakiwa kutoa wahitimu ambao wanakidhi soko la ajira. "Nawasihi mafanikio ambayo mmeyapata kwa miaka 55, endeleeni kuwa kitovu cha kutoa elimu bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salam kiongoze wengine wafuate," alisema Rais Kikwete ambaye pia ni miongoni mwa wahitimu waliosoma chuoni hapo katika miaka ya 1970. 

#HabariLeo