Burundi imepiga marufuku makundi 10 ya kutetea Haki za Binadamu



Burundi imepiga marufuku makundi 10 ya kutetea Haki za Binadamu, huku muungano wa kutetea haki na maslahi ya waandishi habari pia ukivunjwa. Serikali inayalaumu mashirika hayo 10 kwa kueneza chuki nchini Burundi na kuchochea fujo na kutishia Usalama wa Taifa.

Mashirika matano kati ya kumi yamevunjwa kabisa, likiwemo la Protection of Human Rights and Detained Persons (APRODH). Shirika hilo lilikuwa likiongozwa na mwanaharakati Pierre Claver Mbonimpa, aliyehamia barani Ulaya mwaka jana baada ya kunusurika jaribio la kuuawa lililotekelezwa na watu waliokuwa na silaha katika mji mkuu Bujumbura.