Wasanii anaowakubali kwa kuimba Live



Ukiambiwa utaje orodha ya wasanii wa Bongo Flava waliobobea kwenye muziki wa live, huwezi kuacha kumtaja Banana Zorro. Muimbaji huyo anayetoka kwenye familia ya muziki – baba yake akiwa Mzee Zahiri Zorro, gwiji wa muziki wa dance, Banana amejikusanyia weledi na uzoefu mkubwa wa kuimba live kupitia bendi yake, B Band. Na sasa akiongea na mtangazaji wa Kings FM, Prince Ramalove, muimbaji huyo wa Nzela amewataja wasanii wawili wa Bongo Flava anaowakubali kwa kuimba live. 

Wasanii aliowataja ni Barnaba na Ruby. Wawili hao licha ya kuwa na uwezo katika kuimba muziki jukwaani, kwa sasa wanafanya vizuri redioni na nyimbo zao ‘Lover Boy’ na ‘Walewale’ huku Ruby akidaiwa kufanya maajabu kwenye msimu mpya wa Coke Studio Africa. Kwa upande mwingine, Banana amekiri kuwa muziki wa live unazidi kukua Tanzania, kitu anachosema alikuwa akikipigania kwa kipindi kirefu.