Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete na Waziri mkuu wake wa zamani Edward Lowassa jana walikutana uso kwa uso kwa mara ya kwanza na kusalimiana kwa kushikana mikono, tangu walipopishana kimtazamo miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Wawili hao walionekana kutofautiana kimtazamo wa kisiasa wakati wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kupitisha majina matatu ya wagombea urais kupitia chama hicho.
Kabla ya kuanza kwa kikao hicho ambacho wajumbe waliimba pambio la kuwa na imani na Waziri Mkuu Mstaafu huyo badala ya Mwenyekiti wa zamani wa chama huyo, jina la Lowassa lilikuwa limekatwa kwenye mchujo wa kuwapata tano bora Julai mwaka jana.
Uamuzi huo ulimfanya Lowassa aamue kuhamia upinzani ili kugombea Urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, akijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huku akiungwa mkono pia na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Katika kampeni hizo Lowassa aliishambulia waziwazi rekodi ya utendaji wa Kikwete, ambaye naye alijibu mapigo katika mikutano ya kampeni ya kumnadi mgombea wa CCM wakati huo, Rais Magufuli.
Lakini hatimaye jana wakakutana katika kuaga mwili wa aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, kwenye Viwanja vya Karimjee jijini.
#Nipashe