CHUO CHAFUNGWA BAADA YA KUTUNUKU SHAHADA WANAFUNZI WALIOSOMA KWA SIKU 60

Baraza la Taifa la Elimu ya Juu nchini Uganda (NCHE) limebatilisha kibali cha Chuo Kikuu cha Busoga kufuatia kitendo cha wanafunzi zaidi ya 1,000 kutoka Sudan Kusini kudahiliwa na kuhitimu shahada ya awali kwa siku 60 (miezi miwili).



NCHE imefikia uamuzi huo baada ya kufanya uchunguzi kuhusu sakata hilo baada ya Idara ya Elimu nchini Sudan Kusini kuliomba baraza hilo kuchunguza udahili wa wanafunzi hao ambao wengi wao ni wafanyakazi wa serikali na watumishi wa jeshi la nchini hiyo. Uchunguzi ulitakiwa kufanyika katika matokeo yao ya kila mhula, matokeo katika kila somo, na malipo ya ada katika miaka mitatu iliyopita.

Aidha, Sudan Kusini iliomba uchunguzi ufanyike kama kuna uhusiano wowote uliopo kati ya Chuo Kikuu cha Juba na Chuo Kikuu cha Busoga, kuangalia mahudhurio ya wanafunzi katima mihadhara na pia wakaomba kuzuiwa kwa wanafunzi ambao hawakuwa na sifa za kuhitimu masomo.

Mbali na wanafunzi hao wa Sudani Kusini, imefahamika pia kuna wanafunzi 50 wa Nigeria katika sakata hilo. Chuo hicho kiliwahi kukumbwa na kashfa kama hiyo mwaka 2012 ambapo watumishi wanne wa chuo walisimamishwa kwa kusababisha baadhi ya wanafunzi kutunukiwa shahada wakati hawakuwa wakistahili.

Uchunguzi uliofanyika uligundua kwamba nyuma ya sakata hili kuwa watu wenye uwezo kwani kwa miezi miwili ambayo wanafunzi hao wamesoma, chuo hicho kilijipatia USD milioni 1 (TZS bilioni 2.2) kufuatia kila mwanafunzi kulipa zaidi ya ada inayotakiwa.