Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye amekuwa kimya kuzungumzia sakata linaloendelea ndani ya chama hicho likimuhusisha Profesa Ibrahim Lipumba, jana aliondoa ukimya na kueleza kuwa kinachoendelea ni mpango ulioandaliwa wa kuvuruga jitihada za chama hicho za kudai haki, lakini hautafanikiwa.
Pamoja na hayo, Maalim Seif, aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), amesema kuna jitihada alizoziita za mwendokasi za jumuiya ya kimataifa kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar. Maalim Seif alisema hayo jana wakati akitoa salamu zake fupi kwa mamia ya waumini na wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika Msikiti wa Kihinani, Wilaya ya Magharibi A.
CUF iko kwenye mvutano wa uongozi kutokana na Profesa Lipumba kushika ofisi kuu za chama hicho zilizoko Buguruni jijini Dar es Salaam akisema kuwa ndiye mwenyekiti halali wa chama hicho baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kutoa msimamo na maoni ya ofisi yake kuhusu sakata hilo.