SERIKALI ya Rais Dk. John Magufuli imetwaa nyumba 5,696 zilizokuwa zikimilikiwa na halmashauri za majiji, miji na wilaya na sasa zitakuwa chini ya umiliki wa serikali kuu.
Uamuzi huo ambao ni pigo kwa halmashauri mbalimbali nchini, hasa zinazoongozwa na vyama vya upinzani, ulifanywa rasmi Julai 10 mwaka huu.Tayari Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, ameandika barua kwenda kwa wakuu wa mikoa yote nchini kuhusu uamuzi huo kwa ajili ya utekelezaji.
Barua hiyo imeandikwa Agosti Mosi, mwaka huu.Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba EA.137/176/011/40, Waziri Lukuvi anaeleza kuwa nyumba hizo sasa zitasimamiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa niaba ya serikali.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya maamuzi yafuatayo: Amehamisha umiliki wa nyumba 5,696 zilizotajwa kwa GN (tangazo la serikali) namba 323 ya mwaka 1991 kutoka serikali za mitaa kwenda serikali kuu kuanzia tarehe 1o Julai 2016,” inasema barua hiyo.
Katika barua yake, Lukuvi ameainisha kuwa Rais ameagiza uhakiki wa nyumba zote hizo ufanyike kwa mujibu wa GN hiyo ya mwaka 1991 ili ‘isipotee’ nyumba hata moja na maeneo yenye nyumba hizo yapimwe rasmi.
Ameagiza pia kwamba baada ya upimaji nyumba hizo zipewe hati moja kwa jina la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na watu waliovamia maeneo ya nyumba hizo kwa shughuli zozote waondolewe haraka