Mabasi ya mwendokasi yaanza ruti ya Muhimbili

KAMPUNI ya Usafiri wa Mabasi yaendayo Haraka (Udart) kuanzia leo inaanzisha huduma za usafiri wa mabasi hayo kutokea Gerezani hadi Muhimbili. Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salama na Meneja Uhusiano wa Udart, Deus Buganywa.



Buganywa alisema mabasi yataanzia Gerezani kupitia Msimbazi A na B, Fire na baadaye kuingia kwenye barabara za kawaida kuelekea Muhimbili. “Nauli itabaki ile ile, kwa abiria anayetoka Mbezi, Kimara, Ubungo, Morocco au Kivukoni akifika Fire, Msimbazi au Gerezani, ataunganisha na basi la Muhimbili kwa nauli ile ile hatahitaji kuongeza nauli. Buganywa alisema huduma zitaanza saa 11 alfajiri na mabasi manne yataongezwa kulingana na mahitaji. “Lengo la huduma hizi ni kuwawezesha abiria wetu kufika Muhimbili bila usumbufu. “Basi zitakazotumika ni zile za trunk (njia kuu) na si zile za feeder kutoka Gerezani mpaka Fire abiria watatumia milango ya kulia kuingia na kutoka kwenye vituo kama yanavyofanya mengine, baada ya Fire watatumia mlango wa mbele kushoto,” alisema.

Alipoulizwa kwa nini basi hizi zinaanzia Gerezani na si kwenye vituo vikubwa, Buganywa alisema lengo ni kuwawezesha watu wa kutoka njia zote waunganishe mabasi Fire. “Njia hiyo itatoa mwanya kwa abiria wa njia zote waweze kuunganisha na pia Fire hakuna pa kugeuzia ndiyo maana tukaamua yaanzie Gerezani yanapoweza kugeuzia ambapo pia ni jirani na Fire,” alisema Buganywa. 

#HabariLeo