Anaandika GODLISTEN MALISA: Kwanini SUMATRA imefuta route za Posta Mbezi kwa daladala za kawaida?

Naomba kusaidiwa uelewa. Kwanini SUMATRA imefuta route za Posta Mbezi kwa daladala za kawaida? Sasa hivi kama unatoka Posta kwenda Mbezi hakuna daladala zaidi ya Mabasi yaendayo kasi. Utakwenda nayo ukifika Kimara safari inaisha, unapanda daladala za kawaida kutoka Kimara kwenda Mbezi. Nasikia serikali imefanya hivi ili kuondoa ushindani kwa mabasi yaendayo kasi. Yani waachiwe wenyewe wadominate njia maana walianza kupoteza wateja na hivyo kujiendesha kwa hasara.



Kama ni kweli hii si haki kabisa kwa walalahoi ambao usafiri wao mkubwa ni daladala. Wale wenye magari binafsi watapata ahueni kwa kupunguziwa foleni ya daladala, lakini walalahoi wataumia sana.

Kwa mfano mlalahoi wa Mbezi alikua akitaka kwenda Kariakoo anapanda gari moja (TZS 400/=). Lakini sasa hivi atalazimika kupanda magari mawili. Atapanda Mbezi Kimara 400/= kisha atapanda mwendokasi Kimara Kariakoo 650/=. So badala ya kufika Kariakoo kwa 500/= kama zamani, saivi atafika kwa 1,050/=. Ongezeko la 650/=.

Ngoja nikupe mfano wa pili. Mlalahoi wa Mbezi ambaye ndugu yake amelazwa Muhimbili alikua anapanda gari moja tu kwa 400/= hadi Muhimbili kwenda kumuuguza ndugu yake. Lakini kwa utaratibu mpya wa sasa atalazimika kupanda gari 3. Moja la kutoka Mbezi Kimara 400/=, kisha apande Mwendokasi Kimara Posta 650/= ashuke Fire. Halafu asubirie magari ya Muhimbili yatokayo Buguruni au Temeke apande kwa 400/=. Jumla 1,450/=. Ongezeko la 1,050/=.

Gharama hizi za nauli zinapanda wakati hali ya uchumi ikizidi kudorora. Yani mtu aliyekua anaenda Muhimbili kwa TZS 400/= sasa hivi anakwenda kwa TZS 1,450/=. Wakati huo anamuuguza ndugu yake, na yupo mtaani mwaka wa pili hana ajira maana serikali imezuia kuajiri kwa muda.

Nadhani serikali ina haja ya kutizama upya jambo hili. Kazi ya serikali ni kuboresha maisha ya wananchi, na sio kuyafanya yazidi kuwa magumu.!

Malisa GJ