MWANAMITINDO wa kimataifa anayefanya shughuli zake nchini Marekani, Flaviana Matata, amepongeza ushindi wa Bilionea Donald Trump dhidi ya Hillary Clinton kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais nchini humo.
Akizungumza na MTANZANIA, Flaviana Matata alisema yeye hakuwa shabiki wa masuala ya siasa nchini humo, ila alikuwa anavutiwa na sera za mgombea wa Chama cha Democratic, Hillary Clinton na ushindi wa Chama cha Republican kupitia Donald Trump, ameupokea kwa mshtuko kama ilivyo kwa watu wengi. “Sikuwa shabiki wa Trump ila ushindi wake umenifanya nikubali japo sikutegemea kutokana na kufanya kampeni chafu, nilipenda sana sera za Hillary na nilikuwa nataka ashinde ili aweke historia ya mwanamke wa kwanza kuiongoza dunia,” alisema Flaviana.
Kuhusu hofu iliyotawala kwenye mitandao ya kijamii juu ya watu wasio wa taifa hilo kupata misukosuko kufuatia vitisho alivyowahi kuvitoa Donald Trump kwenye kampeni zake, Flaviana Matata alisema uraisi ni taasisi, hivyo hata kama ana maamuzi yake ni lazima utafuata taratibu utakazozikuta ofisini. “Unaweza kuwa na mipango yako mibaya lakini ukishakalia kiti cha urais, ni lazima utaongoza kwa kufuata taratibu utakazozikuta. Si rahisi kufanya maamuzi ya kukurupuka, unajua ukiwa Rais wa Marekani unakuwa kiongozi wa dunia, hivyo najua Trump atakuwa makini kwa hilo,” alisema Flaviana.
Chanzo: #Mtanzania