Magufuli afichua siri kuitumbua Bodi TRA

RAIS John Magufuli amefichua siri ya hatua yake ya kuitumbua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Amesema alilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya bodi hiyo kuidhinisha Sh bilioni 26 kupelekwa kuwekwa kwenye akaunti maalumu katika benki kadhaa za biashara.

Magufuli


Bodi hiyo ilitoa idhini ya kupelekwa fedha hizo katika benki hizo wakati kuna agizo la Rais la kupiga marufuku kwa taasisi za umma, mashirika ya umma, idara za serikali, wakala na wizara kuweka fedha zao katika benki za kibiashara.

Fedha hizo zinatakiwa zifunguliwe akaunti katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Jumapili iliyopita asubuhi, Ikulu ilitangaza kwamba Dk Magufuli ameivunja Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, na saa chache akateua Naibu Kamishna Mkuu mpya. Ikulu bila kueleza sababu, ilisema kwamba Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Bernard Mchomvu na kuivunja bodi nzima.

Aidha, pamoja na kuivunja bodi hiyo alimteua Charles Kichere kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, kuziba nafasi iliyokuwa wazi kwa mwaka mmoja baada ya Dk Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa akishikilia wadhifa huo Lusekelo Mwaseba. “Uteuzi wa Mwenyekiti mwingine wa Bodi ya Wakurugenzi wa TRA na Bodi ya Mamlaka hiyo utatangazwa baadaye,” ilieleza taarifa ya Ikulu iliyotolewa Jumapili asubuhi sana.

Kwa mujibu wa shajala ya mwaka huu ya TRA, wajumbe wa bodi hiyo ambayo waliteuliwa mwaka 2014 na walitakiwa kuhudumu hadi mwaka 2017 na maeneo waliokuwa wakifanyakazi wakati wakiteuliwa kwenye mabano ni Shogholo Msangi (Kamishna Msaidizi wa Sera, Wizara ya Fedha), Khamis Omari (Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Zanzibar) na Dk Philip Mpango (akiwa Katibu Mkuu Tume ya Mipango). Kwa sasa, Dk Mpango ni Waziri wa Fedha na Mipango.

Wengine ni Profesa Beno Ndullu (Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania-BoT), Assaa Ahmad Rashid (Katibu Wizara ya Katiba na Sheria Zanzibar), Josephat Kandege (Mbunge Kalambo – Rukwa), Dk John Mduma (Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Utafiti wa Uchumi na Sera Chuo Kikuu cha Dar es Salaam -Udsm), Dk Nsubili Isaga, (Mhadhiri Chuo Kikuu cha Mzumbe), na Rished Bade (akiwa Kamishna Mkuu TRA). Katibu wa Bodi hiyo alikuwa Juma Beleko (TRA).