Matapeli watumia Jina La Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam (Paul Makonda) KUTAPELI watu

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema Mkurugenzi wa Kampuni ya Group Six International, raia wa China, Jensen Hung (39) ametapeliwa zaidi ya Sh milioni 22 na mtu aliyejiita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Wakazi wa jijini humo na wageni wametahadharishwa kuwa makini.



Kwa mujibu wa Polisi, kumeibuka wimbi la wahalifu wanaotumia mbinu hususan majina ya viongozi wa serikali au watu mashuhuri na kujipatia fedha kwa njia ya kitapeli kinyume cha sheria za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema matapeli hao wamekuwa wakitumia zaidi majina ya viongozi haswa jina la Mkuu huyo wa Mkoa kwa lengo la kujipatia fedha.

“Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa raia wa kigeni kwamba kuna baadhi ya wahalifu wanaotumia vibaya jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa watoe kiasi cha fedha za kigeni na fedha za kitanzania kwa madai ya kuwasaidia wanafunzi kupata vyuo huko nchi za nje kama Ufilipino,” alisema Kamanda Sirro.

#HabariLeo