PWANI: Ateseka kutunza familia ya wasioona 7

MWAJUMA Nasoro, mkazi wa Simbani wilayani Kibaha mkoani Pwani, yuko kwenye wakati mgumu wa kulea familia ya watu saba, ambao hawaoni.



Mwajuma hana shughuli yoyote ya kumuingizia kipato, zaidi ya kulima vibarua kwa ajili ya kujipatia chakula.
Mama huyo alikuwa ameolewa na Nasoro Abdala (80), ambaye naye haoni. Hata hivyo, miaka michache iliyopita waliachana, hivyo kubaki na mzigo mkubwa wa kuilea familia hiyo, ambapo wanajipatia riziki katika mazingira magumu ya kulima, kuchoma mkaa na kushona mikeka.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha, Mwajuma alisema licha ya kuwa na familia hiyo yenye watoto wasioona wakiwemo wajukuu wawili, hana msaada wowote kutoka serikalini, mashirika au watu binafsi.
Watoto wa mama huyo wasioona ni mume wake, Abdala Nasoro na watoto Laila Nasoro (30), Aziza Nasoro (26), Asia Nasoro (21), Kasimu Nasoro (18) na Latifa Nasoro.

Wajukuu zake ni Majidi Maulid (11), anayesoma darasa la 3 mkoani Tanga kwenye Shule ya Wasioona ya Irente; na Tariq ambaye bado ni mdogo akiwa chini ya miaka mitano; na alipopimwa alionekana hana uwezo wa kuona mbali na anahitaji matibabu ili asije kushindwa kuona.

Mwajuma alisema kuwa watoto wake wanne pamoja na wajukuu wawili, hawaoni pamoja na mume wake, ambaye hawaishi pamoja kwa sasa. Alisema anashirikiana na mwanawe mmoja ambaye anaona na mkwe wake, ambao wote hao wanategemea kufanya shughuli za kulima vibarua ili kujitafutia riziki ya kila siku.

Alisema watoto wake, wamekuwa wakipata ulemavu wa kutoona katika mazingira ya ajabu bila kujua sababu. Alisema wamekuwa wakizaliwa wazima, lakini wanapofikia umri fulani, wanapoteza uwezo wa kuona.

#HabariLeo