Tume ya Mufti yafichua ufisadi Bakwata

TUME iliyoundwa na Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakar Zubeir kufuatilia mali za Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) imekabidhi ripoti ya awali kwa mufti huyo huku ikiainisha baadhi ya mali za Waislamu zilizoporwa kwa hila.



Hata hivyo, tume hiyo haikuweka wazi mali walizobaini kuporwa na kueleza kuwa jambo hilo litafanywa na Mufti mwenyewe kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kutoa taarifa za ripoti hiyo. Akizungumza wakati wa kukabidhi ripoti hiyo katika Ofisi za Makao Makuu ya baraza hilo, Kinondoni jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Shehe Abubakar khalid alisema tume hiyo imefanya kazi kubwa hadi kukamilisha ripoti hiyo ya kwanza.

Shehe Hali alisema tume hiyo ilipewa miezi mitatu, lakini kazi hiyo imekuwa ni ngumu hasa kwa kuzingatia kuwa baraza hilo lina mali nyingi nchini kote na shughuli za tume hiyo ilikuwa ni kuhoji wahusika kwa mikataba waliyoingia. “…Ilikuwa ni tabu kuwapata kwa nafasi zao , tumefanikiwa kukamilisha ripoti ya kwanza kwa baadhi ya mali tu na mikataba ya mkoa wa Dar es Salaam, shughuli nyingine zitaendelea baadaye,” alisema Shehe Khalid na kuongeza kuwa ripoti hiyo waliyowasilisha ni nusu ya ripoti ya awali ya kazi ya Dar es Salaam na wataendelea katika mikoa yote hadi watakapokamilisha na ndio sababu ya kuomba waongezewe muda na wanamshukuru Mufti kwa kuwakubalia jambo hilo kwa kuwaongeza miezi mitatu mingine.

Alisema walipewa hadidu za rejea zilizokuwa zikiwaeleza kufuatilia viwanja, majengo pamoja na mali nyingine zilizokuwa zikimilikiwa na Waislamu na ndilo walilolitekeleza. Naye Mjumbe wa tume hiyo, Shehe Hamis Mataka alisema tume hiyo haina mamlaka ya kueleza kilichomo ndani ya ripoti hiyo, bali mufti ndio mwenye mamlaka ya kueleza yaliyomo na kuyafanyia kazi.

Alisema Mufti alitoa hadidu za rejea saba ambazo ni kufuatilia mali za baraza hilo, kuangalia hesabu za baraza, kuangalia namna ya kuboresha mifumo pamoja na mengine. #HabariLeo