Dar es Salaam. Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa), imetoa tahadhari kwa Serikali na Watanzania kupunguza matumaini kwenye manufaa ya gesi asilia huku ikipendekeza kuanzishwa kwa sekta endelevu itakayokuwa mbadala wa rasilimali hiyo.
Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti wa Repoa, Dk Abel Kinyondo alisema matumaini yaliyopo ni makubwa ikilinganishwa na uhalisia kwani makosa yaliyofanyika ni kutoa nafasi kubwa kwa Watanzania kushiriki katika rasilimali hiyo wakati hawana uwezo wa kutosheleza mahitaji na ubora unaohitajika.
Kabla ya kanuni kukamilika, Sera ya Ushirikishaji na Uwezeshaji Wazawa Tanzania (LCP) ya mwaka 2014, Sera ya Gesi Asilia ya 2013 na Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Gesi Asilia ya 2015, Serikali iliweka mkakati wa kuhakikisha wazalishaji na kampuni za ndani zinanufaika kwa asilimia 25 wakati wa uzalishaji.
Akizungumza wiki iliyopita katika mafunzo ya uchambuzi wa masuala ya uchumi na mikataba ya gesi na mafuta kwa wanahabari, Dk Kinyondo alisema kinachoweza kusaidia ni Serikali kuongeza kodi na kupunguza ushiriki wa LCP kwa Watanzania ili kuepuka wajanja wachache watakaojinufaisha wakati wa uzalishaji. #mwananchi