LOWASSA AZUIWA KUFANYA MKUTANO MKOANI SIMIYU, ATISHIWA KUKAMATWA

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA Edward Lowassa amezuiwa na uongozi wa serikali ya mkoa wa Simiyu kufanya mkutano uliokuwa na lengo la kuzindua Operesheni Kata Funua iliyotangazwa na Chama cha Demokrasia na Manendeleo (CHADEMA) kuwa itafanyika kila kata na kila kijiji.

Lowasa


Uzinduzi huo ulipangwa kufanyika Desemba 5 mwaka huu huku Lowassa akiwa ndiye kiongozi aliyepangwa kufanya uzinduzi huo mkoani Simiyu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga alisema kuwa wamezuia uzinduzi huo kutokana na uzinduzi huo kuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.

Kiongozi huyo alisema kuwa moja ya ajenda zilizozungumza katika vikao vya CHADEMA vya Novemba 30 na Desemba 1 mwaka huu ni pamoja na kuanzishwa mkakati wa kushawishi wananchi wa Simiyu wagomee shughuli za maendeleo.

Aidha, uongozi wa mkoa ulisema kuwa utawajulisha CHADEMA kuhusu zuio hilo na kama Lowassa atafika Simiyu kwa ajili ya uzinduzi huo basi atakamatwa na kuchukuliwa hatua.

Chanzo: Majira