Mukandala aongezewa muda Chuo Kikuu cha Dar es salaam

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye ni Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete baada ya mashauriano ameafikiana na Rais John Magufuli kuongeza muda wa Makamu Mkuu wa chuo hicho wa sasa, Profesa Rwekaza Mukandala kwa muda wa mwaka mmoja.



Katika taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari jana, Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Peter Ngumbullu alisema uamuzi huo unaanza mara moja.

Ngumbullu alisema muda wa Profesa Mukandala ulimalizika Desemba 4, mwaka huu.

Profesa Mukandala aliteuliwa kwa kipindi cha sasa cha miaka mitano kilichoanza Desemba 5, 2011 na kumalizika Desemba 4, mwaka huu.

Profesa Mukandala alisema alikuwa tayari ameshajitayarisha kwamba juzi angekabidhi madaraka hayo kwa mtu mwingine, lakini kwa imani waliyokuwa nayo uongozi wa chuo hicho uliridhia aendelee kwa mwaka mwingine. “Viongozi wa chuo hiki wakishirikiana na Rais John Magufuli wamekuwa na imani na mimi na kuniongezea mwaka,” alisema Profesa Mukandala. 

#HabariLeo