Mzee wa Upako |
Wiki mbili zilizopita, taarifa kwenye vyombo vya habari zilisema kwamba Mchungaji Lusekelo alikwaruzana na majirani zake huku akidaiwa kuwa alikuwa amelewa jambo ambalo lilifanya achukuliwe na kuhojiwa na polisi.
Lakini, tangu kuibuka kwa tukio hilo alikataa kulitolea ufafanuzi licha ya kutafutwa na vyombo vya habari, hata pale alipohudhuria ibada kanisani kwake aliwaambia waumini wake hatalizungumzia na badala yake alidonoadonoa baadhi ya matukio.
Alipokwenda kanisa kwake kwa mara ya kwanza Novemba 25, Mchungaji Lusekelo alisema; “Kuna kitu nilikuwa nataka nikiseme, lakini sitakisema ili waendelee kusema haohao waliokuwa wanasema.Wakawaulize wenyewe. Nimeyaona magazeti hapa, ooh Mzee wa Upako, ooh Mzee wa Upako, sisemi. Sasa leo yupo hapa, na kwa taarifa yao watashindana sana, lakini hawatashinda. Hii ni kama kumpiga chura teke.” Lakini, Novemba 28, Mchungaji huyo akajibu baadhi ya hoja akisema kwanza, maneno aliyotumia ambayo ni mshenzi, mpumbavu na mjinga siyo matusi kwani yameandikwa kwenye Biblia. Pili, watu hao ndiyo walianza kumtukana yeye baada ya kuwauliza wanatafuta nini eneo la getini kwake.
Hoja nyingine alisema watu hao hawakuwa jirani zake kama inavyodaiwa kwani mtaani kwake wanaishi kama majambazi kutokana na mazingira ya kutofahamiana.
Jana, Mchungaji Lusekelo akiwahubiria waumini wake alidonoa tena eneo jingine linalohusiana na tukio hilo, kwamba wanaodai alikuwa amelewa pombe, waeleze alikunywa pombe gani na baa gani.
Akikaribishwa kwa wimbo wa kuabudu uitwao, ‘Nina haja nawe’ kabla ya kuanza kumtunza kwa sadaka, Mchungaji Lusekelo alisema watu wanaotuhumu kuwa alilewa, wanatakiwa kueleza alikunywa pombe gani na alikunywa akiwa eneo gani.
#Mwananchi