AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA MITATU KWA KUGHUSHI CHETI

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara, imemhukumu muuguzi Irene Machagge, kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya sh 600,000 baada ya kumtia hatiani kwa kughushi cheti cha elimu ya sekondari na kukitumia katika ajira.

Taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa vyombo vya habari ilisema khukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Karim Mushi baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi wane wa upande wa mashataka na mshtakiwa.

Akitoa adhabu hiyo, Hakimu Mushi alisema amezingatia utetezi wa mshtakiwa, hivyo kumhukumu kulipa faini ya sh 500,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kwanza, na la pili kulipa faini ya sh 100,000 au kwenda jela miaka mitatu.

Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba 15, 2015 akikabiliwa na mashataka mawili ya kughushi cheti cha elimu ya sekondari na kukitumia kujipatia ajira ya uuguzi katika Hospitali ya Mkoa wa Mara.

Ilidaiwa mahakamani na upande wa mashtaka kuwa kati ya Mei na Septemba, 2009 alighushi cheti cha kuhitimu Shule ya Sekondari ya Forodhani mwaka 1995. Na septemba 3, 2009 aliwasilisha cheti hicho kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara na kuajiriwa kama muuguzi katika hospitali ya Mkoa.

Hata hivyo, mshtakiwa aliiomba Mahakama imuonee huruma kwa kuwa ana ujauzito na ana ugonjwa ambao haumruhusu kukaa kwenye eneo lenye joto kali, hivyo alilipa faini ya sh 600,000 na kukwepa kwenda jela.