MAOFISA WA CRDB KUWAJIBISHWA UFUNGUZI WA AKAUNTI YA MAAFA



Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Charles Kimei ameagizwa kuwachukulia hatua watumishi wa benki hiyo walioshiriki kuanzisha akaunti nyingine yenye jina linalofanana na akaunti rasmi ya ‘Kamati ya Maafa Kagera’ kwa lengo la kujipatia fedha.

Agizo hilo limetolewa na Rais John Magufuli aliyesema vigogo wawili wa Serikali mkoani Kagera wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kufungua kinyemela akaunti hiyo.

Watuhumiwa waliofukuzwa kazi na kukamatwa na polisi juzi, ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera (Ras), Amantius Msole na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba (DED), Stephen Makonda.Akizungumza wakati wa kupokea ndege mpya jana, Rais Magufuli alisema Serikali itahakikisha fedha zote zinazotolewa kukabiliana na madhara ya tetemeko la ardhi, zinafikishwa kwa walengwa na watakaothubutu kuiba watashughulikiwa.

Alibainisha baada ya kutengua uteuzi na kuchukua hatua nyingine dhidi ya Ras, DED na kumsimamisha kazi mhasibu mkuu wa Mkoa wa Kagera, Simbaufoo Swai, amemuagiza Dk Kimei kuwachukulia hatua watumishi wa benki hiyo walioshiriki kuanzisha akaunti hiyo.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alikataa kuzungumzia masuala yanayohusiana na watuhumiwa hao kwa sasa.

#Mwananchi