Majaliwa: Hakuna aliye juu ya sheria

SERIKALI imesema kuwa hakuna mtu aliyekuwa juu ya sheria na mamlaka ya kuwanyanyasa watu wasiokuwa na uwezo kwani Sheria haiangalii nafasi ya mtu.

Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliposimama kwenye Kijiji cha Miono wilayani Bagamoyo mkoani Pwani baada ya wananchi kudai kuwa baadhi ya wafugaji wamekuwa wakipendelewa mara wanapolisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima.

Majaliwa alisema hakuna mtu aliyejuu ya sheria na kwamba watu wanapaswa kuzingatia sheria na wafugaji wanapaswa kufuga mifugo michache ambayo wataimudu na sio kufuga mifugo mingi huku eneo la malisho likiwa dogo.

Alisema kuwa watendaji wa serikali wanapaswa kutopendelea upande wowote ili haki iweze kutendeka na hakuna mtu atakayeonewa kisa uwezo wake ni mdogo.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Saadani kuhusiana na mgogoro wa ardhi uliopo baina yao na Hifadhi ya Saadani alimtaka mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze na Mkuu wa wilaya na watu wa ardhi na kamati ya ardhi ya kijiji kwenda kwa ajili ya kuhakiki mipaka.

Majaliwa alisema kuwa ramani zipo hivyo hakuna sababu ya kugombana kwani kila kitu kinajulikana na haki itatendeka na wananchi hawataweza kuonewa.

Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete alisema kuwa kumekuwa na migogoro mingi ya mipaka katika vijiji ambavyo vinapakana na Hifadhi hiyo hali ambayo imeleta uhasama mkubwa. Ridhiwani alisema kuwa kamati mbalimbali za kusuluhisha migogoro hiyo zimeundwa na bado zinaendelea kufuatilia changamoto hizo hivyo anaamini kwenda kwake kutasaidia kuharakisha kufikia mwisho kwa migogoro hiyo.