Baada ya agizo la Rais John Magufuli kuwataka watumishi wote waliopewa posho za kuhudhuria kilele cha mbio za Mwenge, Madereva na Wasaidizi wa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya mbalimbali nchini ambao walikuwa tayari wamefika Mkoani Simiyu kushiriki sherehe hizo wameeleza kuumizwa na agizo la kurejesha fedha za kujikimu ambazo kiasi walizitumia kwa shughuli husika.
"Sisi hatukuomba kuja Bariadi kwenye sherehe za Mbio za Mwenge wa Uhuru. Tuliambiwa kuja na tukapewa fedha ambazo tumezitumia kwa mujibu wa mahesabu ya matumizi tuliyoandikiwa kwa sababu ilibidi tule na kulala kwenye nyumba za wageni. Hapo sisi kosa letu liko wapi" alisema mmoja wa madereva. "Ilinibidi nimlipe mwenye chumba gharama zote za siku 7 ambazo nilitarajiwa kuishi hapa kama nilivyotumwa kwasababu ya uhaba wa vyumba. Sasa naanzaje kumwambia mwenye hotel anirudishie pesa yangu yote ili nirejeshe ofisini?" aliongezea moja ya wasaidizi wa mkuu wa mkoa.
Hata hivyo, wakati wasaidizi wa viongozi hao wakionesha kuvurugwa na agizo hilo ambalo wanasema limewaingiza hasara ambayo imetokana na kutumwa wafanye wajibu wao, baadhi ya wakuu wa mikoa walikua wameshaanza kurejesha fedha hizo.