MALISA: MIKOPO YA ELIMU YA JUU: JK ALIMALIZA NA 54%, JPM AMEANZA NA 12.5%



By Malisa GJ,

Nimekua nikitafakari suala la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na namna serikali inavyochukua hatua, na kugundua kwamba kumekua na mkanganyiko mkubwa baina ya viongozi wa serikali ambao wamekua wakitoa kauli za kupingana wao kwa wao hali inayozidisha sintofahamu ya suala hili.

Kwa mfano leo Waziri wa Elimu Prof.Joyce Ndalichako ameeleza kuwa idadi ya wanafunzi wliodahiiwa na TCU mwaka huu ni 58,000 na waliokidhi vigezo vya kupata mikopo ni 25,000 tu. Akashangaa na kuuliza iweje wanafunzi 66,000 wakose mikopo wakati waliodahiliwa na TCU ni 58,000 tu? Ndalichako akasahau kuwa si wote wamedahiliwa na TCU, wengine wamepitia NACTE.

Tarehe 19 Oktoba 2016, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) Abdul Razaq Badru alitoa ufafanuzi juu ya idadi ya wanafunzi wa Mwaka wa Kwanza watakaopata mikopo ya elimu ya juu. Katika ufafanuzi wake, Badru alieleza kuwa wanafunzi wa Mwaka wa Kwanza walioomba Mkopo ni 88,000. Kati yao  ni wanafunzi 21,500 tu ndio waliokidhi vigezo.

Haihitaji degree kujua hapa kuna tatizo. Ndalichako anasema waliodahiliwa ni 58,000 lakini Prof.Badru anasema walioomba ni 88,000. Tumuamini nani?? Kama waliodahiliwa ni 58,000 halafu walioomba mkopo ni 88,000 Ndalichako atuambie hao 30,000 wampetoka wapi? Maana kwa maelezo yake it means waliomba mkopo bila kupata udahili jambo ambalo si rahisi.

Ndalichako anashangaa na kujiuliza iweje wanafunzi 66,000 wakose mikopo wakati waliodahiliwa ni 58,000 tu?? Nadhani swali hili Ndalichako alipaswa kumuuliza Badru, kwa sababu Badru ndiye aliyesema wanafunzi 88,000 waliomba mkopo mwaka huu. Na waandishi walioandika habari hii walimnukuu Badru kwa kufanya "attribution". Sasa Ndalichako anaulizaje waandishi waliopewa habari badala ya kumuuliza Badru aliyetoa habari?

Kama Ndalichako anaona "figures" hazipo sawa amuite Badru amuulize ametoa wapi idadi ya wanafunzi 88,000 wakati idadi aliyonayo yeye kama Waziri ni 58,000?? Kuwalaumu waandishi wa habari hakuwezi kumsaidia Ndalichako kwa sababu wao sio chanzo cha habari hiyo.

Lakini watanzania wanajiuliza kati ya Badru na Ndalichako nani aaminiwe? Wote ni viongozi wa serikali, wote wanahusika na suala la mikopo ya elimu ya juu, lakini wanajichanganya. Kila mmoja anatoa taarifa yake.

Obviously Badru anaweza kuwa kwenye nafasi ya kuaminiwa zaidi kuhusu suala la mikopo kuliko Ndalichako. Hii ni kwa sababu Badru yeye ndiye "boss" wa bodi ya mikopo. Yeye ndiye anayejua wanafunzi wangapi wameomba, wangapi wana sifa, wangapi wamepewa mikopo na wangapi wamekosa. Ndalichako yeye kama Waziri ni "mwanasiasa tu" na pia ana mambo mengi ya kufuatulia kwenye wizara yake, kwa hiyo suala la mkopo anaweza asilijue vizuri kuliko Badru.

Taarifa ya Ndalichako kwamba wanafunzi 58,000 ndio waliodahiliwa mwaka huu ni ya kutiliwa mashaka. Baraza la mitihani la Taifa (NECTA) mwezi June mwaka huu lilitoa taarifa kuwa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita mwaka huu wenye sifa za kujiunga na vyuo vulikuu ni 60,407 (ingia hapa http://m.ippmedia.com/sw/habari/matokeo-kidato-cha-sita-waliofuzu-kuingia-vyuo-vikuu-ni-hawa).

Wanafunzi waliokua na sifa za kujiunga na vyuo vikuu ambao hawakutokea kidato cha sita mwaka huu walikua zaidi ya 30,000. Hawa ni wale wenye sifa za kusoma shahada (degree) kwa sifa linganifu (equivalent pass), au waliohitimu kidato cha sita miaka kadhaa iliyopita.

Kwahiyo ukichukua wanafunzi 66,407 waliofaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu mwaka huu, ukajumlisha na 33,000 wenye sifa linganifu au waliomaliza kidato cha sita miaka kadhaa iliyopita utapata wanafunzi karibu 90,000. Sasa Ndalichako anasemaje waliodahiliwa ni 58,000 tu?

Badru alieleza kuwa kati ya wanafunzi 88,000 walioomba mkopo mwaka huu, waliokidhi vigezo ni 21,500 tu, na kati ya hao 21,500 tayari Bodi imeshatoa mikopo kwa wanafunzi 11,000 na kwamba idadi iliyobaki watapata hapo baadae kwa kadri vyuo vitavyokua vikifunguliwa.

Kwahiyo kwa mujibu wa Badru wanafunzi walioomba mikopo (wenye sifa na wasio na sifa) mwaka huu ni 88,000 na waliopata hadi sasa ni 11,000 tu. Hii ni sawa na asilimia 12.5% ya waombaji wote. Yani serikali ya JPM hadi sasa imefanikiwa kutoa mikopo kwa 12.5% tu ya wanafunzi wote walioomba.

Mwaka jana ambao ulikua mwaka wa mwisho wa utawala wa JK jumla ya wanafunzi 40,836 walipata mikopo ya elimu ya juu kati ya wanafunzi 76,000 walioomba. Wanafunzi hawa walipata mikopo kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza, Bodi ilitoa orodha yenye jumla ya waombaji 12,282 na awamu ya pili ilitoa mikopo kwa waombaji 28,554. Jumla 40,836.

Kwa hiyo JK katika mwaka wake wa mwisho alitoa mikopo kwa wanafunzi 40,836 kati ya 76,000 walioomba. Hii ni sawa na asilimia 54% ya waombaji wote. Lakini Magufuli katika mwaka wake wa kwanza tu ametoa mikopo kwa wanafunzi 11,000 kati ya 88,000 walioomba. Hii ni sawa na asilimia 12.5% ya waombaji wote.

Kwa lugha rahisi ni kwamba wakati JK alimaliza kwa 54% kwenye suala la mikopo, JPM ameanza kwa 12.5%. Nadhani unaweza kuanticipate atamaliza kwa asilimia ngapi mpaka aondoke madarakani. Leo nimejulishwa kuwa chuo kikuu kishiriki cha Mkwawa, mamia ya wanafunzi wamefungasha virago kurudi majumbani kwao baada ta kukosa mikopo au kupewa viwango visivyokidhi mahitaji yao.

Kwa utaratibu mpya wa "Means Test", mwaka huu Bodi ya mikopo imeanza kutoa fedha za kujikimu kwa madaraja tofauti na ilivyokuwa miaka ikiyopita. Mwaka jana (wakati wa JK) fedha za kujikimu hazikuwahi kutolewa kwa madaraja. Wanufaika wa mikopo walikua walipewa kiasi cha TZS 8,500/= kwa siku kwa ajili ya kujikimu. Logic yake ilikua kwamba wote wanastahili kula, wote wanastahili kulala, wote wanastahili stationeries hata kama viwango vya ada vinatofautiana.

Lakini mwaka huu (utawala wa JPM) fedha za kujikimu zimetolewa kwa madaraja. Haya ni maajabu. Kijana mmoja amenionesha mchanganuo wake amepewa TZS 750/= ya kujikimu kwa siku. Pesa ambayo haitoshi nauli ya kutoka Mabibo Hostel kwenda chuoni Mlimani na kurudi, ndio ameambiwa aitumie kula, kulala, kusafiri, stationeries etc. Seriously?? TZS 750/= pesa ya kujikimu? Hii ni dhihaka.

Halafu Ndalichako anasimama hadharani na kusema kuna watu wanaikatisha tamaa serikali. She cant be serious. Yani umpe TZS 750/= mtoto wa maskini aliyetoka Ngara au Tandahimba, kwamba ndio hela ya kujikimu kwa siku, halafu akilalamika serikali inasema eti inakatishwa tamaa?
Kama kukatishwa tamaa ni kutetea haki za watoto maskini wa Tanzania, acha tuendelee kuikatisha serikali tamaa. Binafsi siwezi kuona mwanafunzi akipewa TZS 750/= kwa siku halafu nikakaa kimya kwa kuogopa kuikatisha serikali tamaa.
Nadhani kuna haja Rais aagize Bodi ya mikopo na Wizara ya Elimu, zipitie upya utaratibu uliotumika kutoa mikopo mwaka huu na wafanye marekebisho haraka iwezekanavyo, au kurudisha utaratibu wa zamani.

Nionavyo mimi serikali ya JPM imeshapigwa "knockout" na serikali ya JK kwenye suala la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. JK alimaliza na 54% (average ya C), JPM ameanza na 12.5% (average ya F). Yani wakati JK alimaliza kwa kupata "daraja C" kwenye mikopo ya elimu, JPM anaanza kwa kupata "daraja F" kwenye suala hilohilo.

Nashauri wizara ya Elimu na Bodi ya mikopo wajipange upya, na wapitie tena "Means Test" na vigezo vya utoaji mikopo mwaka huu, ili wamsaidie "Rais wetu mwema" kusomesha watoto maskini wa kitanzania elimu ya juu. Wanafunzi wote wenye sifa wapate mikopo kama Rais alivyoahidi kwenye kampeni zake mwaka jana.!

Malisa GJ