MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi imetupilia mbali maombi ya mfanyabiashara Freeman Mbowe aliyeomba kurudishwa kwenye jengo la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) baada ya kuondolewa kutokana na kudaiwa kodi ya Sh bilioni 1.3.
Jaji Sivangilwa Mwangesi alitoa uamuzi huo jana baada ya kupitia hoja za pande zote mbili katika shauri hilo na kukubali zilizowasilishwa na mawakili wa NHC. Katika maombi hayo, Mbowe kupitia Kampuni yake ya Mbowe Hotels Limited, alifungua shauri namba 722/2016 dhidi ya NHC, akiiomba Mahakama itoe amri ya kurejeshwa katika jengo hilo kwa madai aliondolewa kinyume cha sheria.
Alidai NHC haikumpa ilani (notisi) kumtaarifu kama anatakiwa kuondoka katika jengo hilo, walimuondoa bila amri ya mahakama, pia Kampuni ya Udalali ya Foster (Foster Auctioneers and General Trad ers) iliyomuondoa katika jengo hilo haikuwa halali.
Aidha, aliiomba mahakama iamuru arudishiwe mali zake zilizochukuliwa na NHC kupitia Kampuni ya Foster kwa madai zilichukuliwa kiholela, pia itoe amri ya kuzuia asisumbuliwe baada ya kurudishwa.
Akitoa uamuzi jana, Jaji Mwangesi alisema mahakama imejiridhisha kuwa hakukuwa na ubia kati ya kampuni hiyo na NHC, bali uhusiano uliokuwepo ni wa mpangaji na mpangishaji. Aidha, mahakama imejiridhisha kuwa NHC ilifuata taratibu zote katika kuiondoa Mbowe Hotels Limited kupitia ilani ya siku 30 iliyotolewa mara mbili na baadaye siku 14.
#HabariLeo