Rais John Magufuli aokoa 1.2 Billion EAC



JITIHADA za Rais John Magufuli katika kubana matumizi yasiyo ya lazima serikalini, ambazo alizihamishia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikiwamo kuzuia safari zisizo za lazima katika jumuiya hiyo, zimewezesha kuokoa zaidi ya Sh bilioni 1.2.

Rais Magufuli ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na aliahidi kuchukua hatua za kubana matumizi yasiyo ya lazima na ikibidi kutumbua watendaji wa EAC, baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo Machi mwaka huu jijini Arusha.

Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko alisema jana jijini hapa kuwa jitihada za kubana matumizi yasiyo ya lazima, zimeokoa Dola za Marekani 588,768 (zaidi ya Sh bilioni 1.2) ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Mei hadi Agosti mwaka huu. #HabariLeo