RAIS John Magufuli atarudisha Mashamba yote ambayo hayajaendelezwa

RAIS John Magufuli ametoa muda wa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara, viongozi na wawekezaji, wanaohodhi ardhi bila kuiendeleza na kuwataka waendeleze maeneo hayo ndani ya kipindi hicho, vinginevyo atatumia mamlaka yake kuwanyang'anya ardhi hiyo.



Dk Magufuli amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwaunga mkono na kuwatengenezea mazingira mazuri ya uwekezaji wafanyabiashara wote watakaowekeza kwa kuzingatia maslahi ya Watanzania.
Rais Magufuli alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999 Kifungu Namba Nne na Tano, kinampatia mamlaka Rais kumnyang'anya mtu yeyote ardhi asiyeitumia kwa mujibu wa sheria na kumpatia mwingine ili aiendeleze.

Alisema hayo katika kijiji cha Mwandege wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani wakati akizindua kiwanda cha kusindika matunda kilichopo chini ya Kampuni ya Food Products mali ya Kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) ya Dar es Salaam. “Natoa mwito awe ni waziri, kiongozi, mwekezaji au hata mfanyabiashara anayejijua kuwa anahodhi ardhi bila kuiendeleza, ahakikishe ndani ya mwezi huu aanze sijui kulima sijui kufanya nini kwa maana ya kuiendeleza baada ya hapo, nitafuata sheria na kuwanyang'anya na kuwapatia wawekezaji wenye kuyaendeleza maeneo hayo,” alisisitiza.#HabariLeo