ZITTO ZUBERI KABWE atabiriwa kuwa Rais ajaye Baaada ya Magufuli

Katika hali siyo ya kawaida katika mtandao wa Facebook moja wa mashabiki wa Zitto Zuberi kabwe ameandika makala ifuatayo, ambayo inamtabiria Zitto Kabwe kuwa Kiongozi wa Nchi wa baada ya Magufuli.



Soma Ujumbe huu

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Zuberi Kabwe, nakutambua kama Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, vilevile nafahamu wazee wa Kigoma walikupa cheo cha uchifu wa Buha na kukuita Mwami Ruyagwa.

Hiyo ni heshima kubwa na imeonesha jinsi gani ambavyo wazee wa Buha, Kigoma walivyo na imani kubwa juu yako. Ni jukumu lako kulinda heshima na imani hiyo. Ishi kama Mwami siku zote ili wasijilaumu kukutuku cheo hicho ambacho kikubwa mno kwa mila na desturi za Buha. Novemba 20, mwaka jana, ulipiga picha ukiwa na Rais John Magufuli pamoja mtangulizi wake, Dk Jakaya Kikwete. Picha hiyo uliiweka kwenye ukurasa wako wa Facebook na kuandika: “Rais wa Nne, Rais wa Tano na Rais wa Sita.”

Tafsiri ilikuwa nyoofu kwamba unajibshiria Urais Rais wa Tanzania baada ya Dk Magufuli. Ni jambo jema na sina shaka na uwezo wako wa kisiasa na kiuongozi. Ulithibitisha ubora wako ukiwa kijana mwenye umri wa miaka 28, siwezi kukupunguzia alama sasa hivi ukiwa na umri wa miaka 40.

Wazungu wana msemo wao kuwa busara hupatikana hasa kwa mtu akishatimiza umri wa miaka 40 na kwamba endapo mtu atafikisha makamo hayo na asiwe na busara basi hatakuwa nazo tena. Hivyo basi, Zitto wewe si kijana tena, hupaswi kufanya makosa ya ujana.

Hata maeneno yako kuwa wewe ndiye Rais wa Sita wa Tanzania, bila shaka yanasababishwa na uhakika kuwa Uchaguzi Mkuu ujao, hautakunyima haki ya kugombea kwa sababu za umri. Uchaguzi uliopita ulikunyima haki hiyo kwa sababu hakuwa na miaka 40 ambayo ndiyo inaruhusiwa kikatiba kwa mtu mwenye kuutaka Urais nchini.
Thibitisha ukubwa wako

Ndugu Mwami Ruyagwa Zitto Kabwe, ilikuwa bahati kwako kuanza kung’ara kisiasa ukiwa kijana mdogo, ukawa mbunge mwenye umri mdogo zaidi kwa wabunge wa kuchaguliwa katika Bunge la Tisa. Kuna mambo ni vema nikujulishe mapema kuwa yapo makosa kadha wa kadha uliyafanya kisiasa lakini hayakuchukuliwa kwa mkazo wake kwa sababu ulitetewa kuwa bado kijana, kwamba uwezo wako wa kisiasa haukupaswa kuwasahaulisha ubinadam wako na kiumri upo kundi gani.

Nitakukumbusha mambo matatu, la kwanza ni lile la mwaka 2012 uliposhutumiwa kuhongwa na makampuni ya mafuta ili uyatetee dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi.

Kupitia tuhuma hizo, uliandika ujumbe mkali wa simu kwa Maswi na kumweleza kuwa hawezi kushindana na wewe, kwani ataumia, kwamba wewe huna kawaida ya kushindwa vita ya kutetea hadhi yako.
Kamati ya Bunge iliyoongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Mlalo, Brigedia Hassan Ngwilizi, ilifanya uchunguzi wake kisha Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda alikusafisha wewe na wenzako mliotuhumiwa kuwa ilikuwa uongo mtupu, zaidi Maswi na Muhongo walionywa kwa kulidanganya Bunge.

Kwa matokeo hayo, naweza kujenga picha ni kiasi gani uliumia pale ulipohisi unasingiziwa tuhuma nzito kama zile. Pamoja na hivyo, ujumbe uliouandika kwa Maswi ulikuwa mkali na wenye kuashiria mapambano binafsi. Wenye kufuatilia siasa wanajua nini ambacho baadaye kilitokea baada ya ahadi yako ya kimapambano. Ushauri kwako ni kuwa baada ya kufikisha umri wa miaka 40, vema uoneshe ukubwa wako. Mashambulizi yatakuja lakini hutakiwi kuyakabili kwa jazba zenye kuonekana. Kila binadam ana hasira ila aliye bora ni mwenye subira.
Upo ujumbe mwingine ambao uliuandika mwaka 2013 kumwelekea Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu. Ulimjibu Lissu kuhusu tuhuma alizokubebesha kuwa ulihongwa magari na mwanasiasa mkongwe nchini, Nimrod Mkono.

Katika majibu yako kwa Lissu, ulimwita yeye ni kifaranga tu wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, jawabu ambalo lilikuwa kali mno. Mwaka huu, ulirejea tena ghadhabu za mapema ulipomshambulia aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga. Ulimwambia kuwa yeye siyo hadhi yako.

Kampeni maarufu dhidi ya Donald Trump anayegombea Urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Republican ni kuwa hatakiwi kupewa mamlaka ya kuongoza taifa hilo kubwa lenye silaha za nyuklia kwa sababu ni mtu ambaye huwa anahamaki na kuchukua hatua kwa uchokozi mdogo wa Twitter.

Kwamba mtu ambaye anachokozeka kwa maneno ya mtandao wa Twitter, anaweza vipi kuaminiwa katika silaha za nyuklia ambazo matumizi yake yatahitaji sahihi yake? Hii ina maana kuwa jinsi ambavyo umekuwa ukichokozeka na kuhamaki, inaweza kuwafanya wapinzani wako wautumie udhaifu huo katika kampeni dhidi yako kama ambavyo inamgharimu Trump kwa sasa. Hivyo kataa kuchokozeka, ni kweli ukichokozwa utakasirika lakini subira yako inapaswa kushinda jazba zako.

Vaa sasa haiba ya  Urais
Umesema wewe ni Rais wa Sita, hilo siyo tatizo ila unachotakiwa kwa sasa ni kuvaa joho la Urais, angalau kwa vitendo vyako na maneno unayotamka, viwe vinafanana na hicho cheo chenyewe. Mvuto wa kisiasa unao, ni kati ya wabunge wachapakazi hilo halina ubishi, wewe ni msomi na unasoma sana vitabu, vilevile umekuwa na maono mapana kuhusu ujenzi wa nchi. Una maarifa mengi ya kiuongozi na katika hilo simuoni wa kubisha. Kote huko kuna alama ya vema, ila bado kuna eneo moja ambalo linahitaji ujenzi, nalo ni la kufanana na cheo cha Rais.

Urais unahitaji maandalizi ya haiba. Kwa ulimwengu wa kisasa hupaswi kujiweka mbali na mitandao ya kijamii hasa Twitter, Instagram na Facebook lakini kupitia huko utashambuliwa tu. Tafadhali usiwe mwepesi wa kujibu mashambulizi.

Tumia mitandao ya kijamii kujenga hoja za kitaalam na za kichambuzi kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi, kisheria, kiutafiti, kiuongozi na kijamii kwa jumla. Usithubutu kutumia mitandao ya kijamii kuonesha hisia zako binafsi hasa unapokuwa umekasirika au kuumizwa. Kunyamaza baada ya kuchokozwa na kuumizwa ni sifa ya kiongozi mkomavu.

Jifunze kutabasamu kwa nje kama Dk Kikwete hata kama ndani unaumia, muige Edward Lowassa asivyojibu mashambulizi dhidi yake au alivyokuwa Rais wa Pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi, ila oneshe uimara wako kama Dk Magufuli au walivyokuwa kwa nyakati zao, Rais Benjamin Mkapa na marehemu Edward Sokoine.
Naufahamu uwezo wako mkubwa wa kujenga hoja, ongeza uwezo zaidi wa kujenga hoja zenye maono kama alivyokuwa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Nayafahamu mapambano yako dhidi ya ufisadi kwa zaidi ya muongo wa pili sasa, endelea kuchukia rushwa na ufisadi kama Dk Magufuli na kama walivyokuwa Mwalimu Nyerere na Sokoine. Chukia na kila mtu aione chuki yako. Imekuwa tabia yako kusifia unapoona panasatahili na kukosoa au kupinga unapoona hapaendi vizuri, endelea hivyohivyo. Kama taifa tunahitaji watu wa kujenga, siyo kwa sababu wewe ni mpinzani ndiyo upinge hata yenye faida. Usiwe mpinzani mwenye ila, baki mpinzani mwenye maono ya kujenga.

Zitto umeoa sasa, na kiongozi mzuri huonekana kuanzia ngazi ya familia. Uwe mume mzuri kwa mkeo na baba bora kwa watoto mithili ya Rais wa Marekani, Barack Obama kwa mkewe Michelle pamoja na watoto wao, Malia na Sasha.

Haiba ya Rais mzuri huonekana kwenye familia yake. Uwe pia mtoto na kaka bora kwenye ukoo wako, ili baadaye utakapowadia muda wa kujinadi, sifa zako njema zitoke ndani na kuwafikia wanajamii wengine. Kiongozi asiyefaa hupingwa na ndugu zake.

Chunga ulimi wako Zitto, pangilia vizuri nyendo zako. Usije baadaye kusalitiwa na maneno yako au vitendo vyako. Ishi ukiwa mtu bora kwenye jamii yako na raia mzuri kwa taifa lako. Msaidie Rais Magufuli kwa mawazo mazuri yenye kuunga mkono, kukosoa au kusahihisha.

Si lazima uwe Rais wa Sita
Una umri wa miaka 40, Uchaguzi Mkuu 2020 utakuwa na umri wa miaka 44, mwaka 2025 utakuwa na miaka 49, hivyo unayo nafasi hata ya kuwa Rais wa Saba au Rais wa Nane, isiwe lazima Rais wa Sita, mwache Mungu afanye kazi yake.

Moja ya hoja zako kuhusu chama chako cha zamani, yaani Chadema ni kuwa hakikuwa kikifuata demokrasia. Onesha uanademokrasia wako kwa kuruhusu mchakato huru wa kuwania tiketi ya kugombea Urais ndani ya ACT-Wazalendo, siyo ujiamulie tu wewe kuwa mgombea.

Zaidi, nakutakia kila heri katika hiyo ndoto kubwa ambayo unaiota kwa ajili ya nchi yako na maisha yako.

Ndimi Luqman Maloto

Karibu sana www.luqmanmaloto.com