GONDWE AAMURU WANAHABARI KUKAMATWA

Mkuu wa mkoa wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe, ameamuru Polisi kuwasweka ndani waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia tukio la kufukuzwa kwa wachimbaji wadogo 3,000 eneo la mlima wa Mazigamba, kijiji cha Nyasa wilayani humo.



Tukio hilo lilitokea Juzi saa 8 mchana ambapo mwandishi wa Clouds Tv Salehe Masoud na mwadishi wa Star Tv MacDonald walikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa saa 8 huku mwandishi wa gazeti hili Nasra Abdallah akifanikiwa kutoroka. 

Agizo la Gondwe kutaka waandishi hao wakamatwe lilitokea baada ya wanahabari hao kufika katika eneo la mgodi na kupata picha ambapo Nyumba zimechomwa na baadhi ya mali kuteketea.
Baada ya wanahabari kufika eneo hilo Polisi waliwaamuru kuzima Kamera zao ambazo hata hivyo zilikuwa hazijawashwa.

Mmoja wa mapolisi alihoji waandishi hao kwanini wamekwenda kwenye eneo hilo bila ruhusa, ivyo kutaka waondoke kwakuwa hawana kibali wala taarifa za ujio wao. Hata hivyo, waandishi hao waliwaeleza Polisi kuwa hawalazimiki kuwa na vibali kufika kwenye matukio ya aina hiyo na kwamba wamekwenda ili kufahamu tukio hilo kwa undani, kwani kuna taarifa kuwa baadhi ya Wananchi wameuawa kwenye operesheni hiyo na maiti zao bado hazijaondolewa.

Baada ya mabishano kama dakiaka 45 ndipo mmoja wa mapolisi hao aliwaongoza waandishi kwa mkuu wa operesheni ambapo nae alikataa kuzungumza chochote na kuwataka waende kwa mkuu wa polisi kituo cha Handeni.

Hata hivyo, waandishi hao waliomba kupiga picha kwanza ndipo waende huko, lakini walikataliwa ambapo polisi huyo aliwaamuru waliopo chini yake kuwaondoa waandishi eneo hilo huku wakiwasindikiza na mitutu ya bunduki na wengine wakiendelea kupiga mabomu.

Muda mfupi baada ya waandishi hao kuondoka gafla waliona gari la polisi kuwafuata kwa nyuma na ndipo walipowaomba madereva wa pikipiki waliokuwa wamewakodisha kuongeza mwendo ili wasikamatwe. Nasra alifanikiwa kukimbika huku Masoud na Mackdonald walikamatwa na kurudishwa katika eneo zilipochomwa nyumba na baadhi ya polisi wakiwaambia wameagizwa na Mkuu wa wilaya Gondwe wakamatwe.

Baada ya kukamatwa waandishi hao walipelekwa kituo cha polisi Handeni ambapo walikaa huko kuanzia saa 8 mchana hadi saa 3 usiku ambapo walitolewa kutokana na juhudi za wahariri akiwemo katibu wa Jukwaa la wahariri Neville Meena kuzungumza na Gondwe.

Akizungumza tukio hilo Gondwe alisema moja ya sababu ya kuwaondoa wachimbaji hao ni kutoweza kulipa kodi na hivyo wamempeleka mwekezaji ili aweze kulipa kodi, jambo ambali wachimbaji wamedai ni taarifa za uongo.

#Chanzo 
TanzaniaDaima